SADC mguu sawa kuangalia uchaguzi wa Tanzania

Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku nane kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, Ujumbe wa Uangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC (SEOM) imejipanga kutathmini misingi ya kidemokrasia nchini ikiwemo haki za binadamu.

SEOM ambayo ilifika nchini tangu Oktoba 12, 2025, imepanga kusambaza waangalizi wake katika mikoa 27 hapa nchini huku ikishindwa kuwafikisha katika mikoa minne ambayo ni Mtwara, Tabora, Shinyanga na Tanga.

Akizungumza na wadau wa uchaguzi wakati wa uzinduzi wa shughuli za uangalizi, leo Oktoba 21, 2025, Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi wa Tanzania, ambaye pia ni Spika mstaafu wa Bunge la Malawi, Richard Msowoya amesema watatathmini ushiriki wa wananchi katika michakato ya kidemokrasia.

Ameongeza kuwa watatathmini endapo wananchi wanafurahia haki za binadamu na misingi ya uhuru kama vile uhuru wa kukusanyika, kuandamana na kutoa maoni. Pia, wataangalia masharti ya mifumo ya kisheria inayohusiana na uchaguzi.

Vilevile, wataangalia na kutathmini hatua za kuzuia rushwa, hongo, upendeleo, vurugu za kisiasa, hofu na ukatili wa mawazo. Pia, watatathmini fursa sawa kwa vyama vyote vya siasa kupata upatikanaji wa vyombo vya habari vya Serikali pamoja na upatikanaji wa taarifa kwa wananchi.

“Ili kutekeleza jukumu lake, SEOM inatathmini na kuangalia yafuatayo, miongoni mwa mengine: Je, mfumo wa kisheria na wa katiba unahakikisha uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kuandamana, uhuru wa kuungana na haki za binadamu.

“Pia, muundo na mfano wa mfumo wa uchaguzi, Mamlaka ya Usimamizi wa Uchaguzi (EMB), Sheria za Uchaguzi na kanuni zake pamoja na asili ya haki za kiraia na kisiasa; na haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni,” amesema Msowoya.

Ameongeza kuwa SEOM itahakikisha kwamba mipaka ya uchaguzi inapangwa kwa njia inayokubalika na wadau, na kama sababu zilizochochea mipangilio hiyo zilikuwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mkuu huyo wa misheni ameeleza kwamba SEOM imekutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi na itaendelea kukutana nao ili kushauriana katika vipindi vyote vya kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Said Saib Mussa amesema uchaguzi wa Tanzania unafanyika kwa kufuata misingi ya demokrasia, kwa hiyo wamewaalika waangalizi wa SADC ili kuwa na uchaguzi huru.

“Hii ni njia moja wapo ya kujipima hapa ndani na ndani ya SADC kwa kuwa sisi ni wanachama. Kazi yao kubwa ni kuangalia uchaguzi na siyo kutoa maelekezo. Hawaruhusiwi kuelekeza jambo,” amesema Mussa.

Naibu katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa katika majukumu yao, SEOM wataangalia namna kampeni zilivyofanyika, wananchi wanavyokwenda kupiga kura na utangazaji wa matokeo, kisha watatoa taarifa yao ya awali.

Ofisa Mwandamizi wa Siasa na Diplomasia – Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika sektretarieti ya SADC, Terry Rose amesema  kufuatia mwaliko rasmi wa Serikali ya Tanzania, Rais wa Malawi, Profesa Arthur Peter Mutharika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Organ ya SADC katika masuala ya siasa, ulinzi na usalama, aliunda Tume ya Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC (SEOM) kwa ajili ya kuja Tanzania kuangalia uchaguzi.

“SEOM itashirikiana na wadau wakuu wa uchaguzi ili kukusanya mitazamo mbalimbali na kuelewa maoni yao kuhusu jinsi uchaguzi unavyofanyika.

“Kwa ajili hiyo, Sekretarieti ya SADC itarahisisha mashauriano kati ya wadau hawa na uongozi wa SEOM, huku waangalizi wetu wakishirikiana moja kwa moja na wadau katika maeneo mbalimbali ya nchi,” amesema.