Dar es Salaam. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema maandamano yatakayofanyika Oktoba 29, 2025 ni kwenda kwenye vituo vya kupiga kura, huku akiwataka Watanzania kumwachia matusi kwani anayabeba kwa niaba yao.
Samia ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu na kuwa hakuna tishio la kiusalama litakalotokea siku ya uchaguzi mkuu na kuwaomba wakichague chama hicho.
Mgombea huyo ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 21, 2025 wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam, kuelekea uchaguzi mkuu.

“Niwahakikishie kuwa Oktoba 29, 2025 kesho kutwa, tokeni muende mkapige kura, ninayeongea hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii. Nataka niwaambie maandamano yatakayokuwepo ni watu kwenda vituoni kupiga kura, hakuna maandamano mengine yatakuwepo, hakuna tishio la kiusalama litakalokuwepo, anayesema ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi,” amesema.
Ameongeza: “Niwaombe ndugu zangu twendeni tukapige kura, baba ukitoka hakikisha unatoka na familia nzima kila aliyeandikishwa. Mabalozi wetu tokeni na watu wenu wote mkapige kura, twendeni mkaheshimishe CCM, tukaiheshimishe Tanzania tukapige kura kwa usalama turudi kwa usalama.”

Amesema aliapa kutumikia Tanzania na ndicho anachokifanya, aliapa kulinda nchi, kujenga utu wa Mtanzania na kuheshimisha na kuwa anapohakikisha watu wanapata maji safi, watoto wanapata elimu na huduma zingine na kuhakikisha usalama wa nchi upo ndiyo kuheshimisha utu wa Mtanzania.
“Ndugu zangu, mengine niachieni mimi, matusi niachieni mimi, nayabeba kwa niaba yenu manabii wetu Bwana Yesu alisulubiwa kwa kukomboa watu kwa ajili ya Mungu, lakini alikuwa anakomboa watu. Muhammad alipigwa mpaka akatolewa meno kwa kufanya kazi ya kukomboa watu kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
“Samia Suluhu aliapa kuitumikia Tanzania na ndicho ninachokifanya, niliapa kulinda nchi na ndicho ninachokifanya, niliapa kujenga utu wa Mtanzania na kuheshimisha utu wa Mtanzania, ndicho ninachokifanya. Ninapohakikisha watu wanapata maji safi, watoto wetu wanapata elimu umeme upo, usalama wa nchi upo, ni kuheshimisha utu wa Mtanzania,” amesema.
Amesisitiza kwamba hana uchungu kubeba kubeba matusi yote yanayotolewa kwa sababu anafanya kazi hiyo, hana uchungu hata kidogo wala hajutii, kwa hiyo amewaomba kura wananchi wa Ubungo na Kinondoni,” amehitimisha mgombea huyo.