Saratani ya matiti kwa wanaume yaongezeka nchini

Dar es Salaam. Tofauti na miaka ya nyuma, saratani ya matiti kwa wanaume imeendelea kuongezeka nchini, baada ya idadi ya wanaobainika miaka ya hivi karibuni kukua.

Taasisi ya Saratani Ocean Road, ORCI imesema kuna ongezeko la saratani ya matiti kwa wanaume kutoka mmoja kati ya wagonjwa wa aina hiyo ya saratani 100 mwaka 2020, kufikia watano kati ya 100 mwaka 2025.

Meneja Huduma za Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa Umma wa Taasisi hiyo, Dk Maghuwa Stephano amesema saratani ya matiti imeendelea kuwa changamoto kubwa duniani huku Tanzania ikishika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani hiyo.

Amesema saratani ya matiti kwa wanaume imeendelea kuongezeka nchini, tofauti na miaka ya nyuma ambapo idadi ya wanaume waliokuwa wakibainika kuwa na ugonjwa huo ilikuwa ndogo.

“Awali kati ya watu 100 wanaofanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti, ni mwanaume mmoja pekee aliyekuwa akikumbwa na ugonjwa huo, lakini sasa takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watu 100, wanaume watano hubainika kuwa na saratani ya matiti,” amesema Dk Maghuwa.

Amesema saratani ya matiti inaweza ikampata mwanaume pia, hivyo kwa sasa kundi hilo nao wanahitajika wajikinge na wafanye uchunguzi wa mara kwa mara ili kujikinga mapema.

Aidha ametoa wito kwa Watanzania hususan wanaume, kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti na saratani nyingine, kwani utambuzi wa mapema ndiyo silaha kuu ya kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

“Tayari inaanza kuongezeka kwa wanaume na tunaendelea kusisitiza wananchi kuacha matumizi ya shisha, tumbaku kwani huko kuna chembechembe nyingi,” amesema.

Manusura wa saratani ya matiti ambaye ni mkazi wa Malamba Mawili Mbezi jijini Dar es Salaam, Ramadhan Rashid Mussa amesema alianza kuumwa kwa muda mrefu na baadaye alifika katika Hospitali ya Mwananyamala, akapimwa kipimo cha ultrasound na moja kwa moja wakamweleza afike Hospitali ya Muhimbili, alikotibiwa na kukamilisha matibabu yake Ocean Road.

Naye Mkurugenzi wa Kinga Ocean Road, Dk Crispin Kahesa amesema katika kuhakikisha kwamba huduma hizo zinapatikana, haziko tu Ocean Road bali zimesambazwa nchi nzima.

“Kuanzia zahanati zetu, vituo vya afya, hospitali za wlaya na mikoa. Lakini pia upatikanaji wa vipimo tunavyo vya CT Scan, X Ray, utrasound kuanzia ngazi za wilaya na mikoa,” amesema Kahesa.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea amesema Ocean Road ni taasisi hivyo Wizara imekuwa ikizitumia takwimu zake kutoa picha ya nchi nzima, “Zimetolewa takwimu za uwiano na si namba kamili. Hii inatoa picha ya hali halisi nchini ilivyo.”

Amesema kuonekana kwa wanaume wengi zaidi hivi sasa inamaanisha kuwa uwezo wa kuweza kubaini kama nchi umekua mkubwa, pia kutokana na uwekezaji mkubwa wa vifaatiba na uwepo wa wataalamu wa kutosha.

“Kilichoongezeka ni utambuzi wa mapema, vituo ni vingi kuanzia ngazi za chini wataanza kuhisi na kuwabaini mapema. Hatua za kwanza anapelekwa rufaa kwa vipimo zaidi na kisha matibabu yanafanyika vizuri na wanapona,” amesema.

Dk Nyembea amesisitiza wanaume waonapo dalili au hali isiyo ya kawaida wafike vituo vya afya karibu na wanapoishi ili kupatiwa vipimo, si lazima waende kwenye hospitali kubwa.

“Wizara ya Afya tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi, kwa sasa magonjwa yasiyoambukiza utaalamu umekua mkubwa ni vema kuzingatia lishe bora na kuwaona wataalamu watabaini mapema na ikigundulika katika hatua za awali inatibika,” amesema.

Wataalamu hao wamesema saratani ya matiti kwa wanaume ni nadra ikilinganishwa na wanawake, lakini wanaume wana tishu ndogo za matiti ambazo zinaweza kupata mabadiliko ya vinasaba (genetic mutations) na kusababisha saratani.

Wametaja vihatarishi kuwa ni pamoja na wanaume wenye viwango vya juu vya homoni ya estrogen wako kwenye hatari zaidi.

Hii inaweza kutokana na unene uliopitiliza, mafuta mwilini hubadilisha homoni za kiume kuwa estrogen. Matumizi ya dawa za kuongeza homoni, mfano kwa matibabu ya saratani ya tezi dume na magonjwa ya ini (kama cirrhosis) ambayo hupunguza uwezo wa mwili kuvunja homoni.

Mabadiliko ya vinasaba kwa wanaume walio na mabadiliko ya jeni BRCA2 wako kwenye hatari kubwa zaidi.

Historia ya kifamilia ya saratani ya matiti au ya ovari inaweza kuwa kiashiria cha urithi wa jeni hizi na hutokea zaidi kwa wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, ingawa inaweza kujitokeza mapema kwa wenye urithi wa vinasaba hatarishi.

Ulevi wa kupindukia kwa pombe nyingi huharibu ini na kuongeza viwango vya estrogen mwilini, hivyo kuongeza hatari ya saratani ya matiti.

Pia wanaume waliowahi kutibiwa kwa mionzi kifuani kwa mfano kutokana na saratani nyingine wanaweza kuathiriwa na baadaye kukuza seli za saratani ya matiti. Pia wenye magonjwa ya korodani au upungufu wa homoni za kiume.