:::::
MWENYEKITI wa Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja ametoa ushauri, akiiomba Wizara ya Elimu nchini ianzishe masomo ya Amani, Uzalendo na Mazingira shuleni kuanzia darasa la awali hadi Chuo Kikuu.
Mgeja ambaye anaongoza taasisi inayojishughulisha na masuala ya haki, Amani na Demokrasia nchini, ametoa ushauri huo mwishoni mwa wiki alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kwanza ya darasa la saba katika shule ya msingi AL WAHAAB PRE, AND PRIMARY SCHOOL iliyopo mtaa wa Sango, Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Amesema suala la Amani, Uzalendo na Mazingira ni muhimu katika ustawi wa nchi na usalama, pia uchumi na maendeleo endelevu kwani watoto wakifundishwa tangu wadogo, watajengeka na kuwa na utamaduni wa kuyaishi maisha yao ya kila siku.
“Utamaduni wa taifa lolote unajengwa, hauoti kama uyoga na waswahili wanausemi kuwa; “Samaki Mkunje Angali Mbichi….” alisema Mgeja.
Kwa mujibu wa Mgeja, chokochoko zinazotokea kote duniani za uvunjifu wa amani na ukosefu wa uzalendo ni tatizo la jamii ambayo haikuandaliwa kujua thamani ya Amani, Uzalendo na Mazingira yao.
Mwenyekiti huyo wa Tanzania Mzalendo Foundation, alisisitiza kuwa Tanzania bado haijachelewa kutoa elimu ya kutambua umuhimu na thamani ya amani, uzalendo na mazingiira, japo kuna viashiria vimeanza kujitokeza kwa baadhi ya watanzania waliolewa amani na kuvimbiwa.
Alisema kikundi hicho cha wachache, kinajidanganya kwani hakitaweza kuichezea amani ya nchi kwa sababu taifa liko salama chini ya uongozi Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hatua nyingine, Mgeja, amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kuiongoza nchi vizuri na kuhakikisha inakuwa na amani na iko katika mikono salama chini ya uongozi wake.
Aidha aliwapongeza viongozi wa dini kwa kuendelea kuhamasisha waumini wao umuhimu wa kutunza amani ya nchi kama mboni ya jicho.
Kuhusu suala la elimu, Mgeja alizipongeza sekta binafsi na taasisi za dini kwa kushirikiana na serikali, kuendelea kuwekeza katika sekta hiyo.
Alisema dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia, elimu ni muhimu kuwekezwa kwa wananchi kama Serikali inahitaji mafanikio ya haraka katika sekta zote.
Alisisitiza kuwa sayansi inahitajika kila mahala, hasa katika masuala ya kilimo, ufugaji, uvuvi, ufundi, biashara viwandani hadi kwenye sekta ya madini.
Kuhusu mabadiliko ya mfumo wa elimu, Mgeja alipongeza Serikali kufanya mabadiliko ya mfumo wa elimu na kuweka mtaala wa amali, jambo ambalo linawafanya vijana wengi wapate elimu ya kujitegemea.
Kuhusu ajira, Mgeja aliwashauri vijana wajitahidi kujiendeleza kiujuzi na kuongeza ufahamu wa lugha za kigeni ambazo ziko sokoni hivi sasa.
Alizitaja lugha hizo kuwa ni Kiingereza, Kichina, Kiarabu na kifaransa kwani zimekuwa bidhaa muhimu katika mafanikio ya ajira na biashara.
Kwa upande wao, wakurugenzi wa Shulw ya Al Wahaab Muslimu Shekhe Mohamed Issa Hilal na Ahmed Abdulrahaman Haluna, wakitoa taarifa kwa nyakati tofauti, wamesema shule hiyo ilianzishwa Mwaka 2019 na mahafari hayo ni ya kwanza tangu kuanzishwa kwake.
Walieleza kuwa shule yao imekuwa na mafanikio makubwa katika malezi mema, elimu bora na maadili na kwamba hii ni dalili tosha kuwa mbegu wanayopanda inakuwa bora na imeendelea kuzaa matunda mema ndani na nje ya Wilaya ya Kahama.