Staa wa zamani wa Simba na Yanga, Alphonce Modest amefariki dunia leo jioni, akiwa nyumbani kwao Kigoma baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.
Taarifa kutoka kwa mdogo wake aliyejitambulisha kwa jina la Agustino Modest amesema: “Kaka amefariki jioni na tunaupeleka mwili wake mochwari, kuhusu kizika bado hatujakaa kikao.
Ameongeza:”Alponse ameumwa kwa muda mrefu kalala kitandani takribani miaka 15, akiwa hawezi kufanya jambo lolote.”

Amesema pamoja na kuumwa, kaka yake alikuwa imara na mshauri mkubwa wa familia hivyo watamkumbuka katika mambo mengi.
“Naamini kupitia kampuni ya Mwananchi marafiki zake watapata taarifa, ambao watakuwa na muda watakuja kumzika.”
Modest amecheza pia kwenye timu nyingine kama vile Pamba, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, wakati wa uhai wake.
Mwanaspoti liliwahi kumfanyia mahojiano kwa kwenda kumtembelea nyumbani kwao Kigoma lilishuhudia mateso yake, ambapo alikuwa hawezi kugeuka, kichwa chake kikiwa kimetazama juu hata akipita mdudu hakuweza kujitoa bila msaada wa ndugu zake.