Takaichi aandika historia ya kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke Japan

Dar es Salaam. Serikali ya Japan imepata Waziri Mkuu mpya aitwaye Sanae Takaichi baada ya kushinda kwa kura 237 bungeni jijini Tokyo, hivyo kuandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.

Takaichi mwenye umri wa miaka 64, ni kiongozi wa chama tawala nchini humo cha Liberal Democratic Party (LDP). Hivyo atakuwa Waziri Mkuu wa 104 wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Tokyo Weekender, Takaichi amechaguliwa kushika wadhifa huo baada ya kushinda kura za Bunge ambapo amepata kura 237 katika Baraza la Chini na kura 125 katika Baraza la Juu, hivyo kupata wingi wa kura unaohitajika katika mabunge yote mawili.

Baada ya ushindi huo Takaichi atakutana na Mfalme Naruhito kwa ajili ya kuapishwa rasmi kama Waziri Mkuu hatua inayoandika ukurasa mpya katika historia ya siasa za nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Al Jazeera, Takaichi, ambaye ni mfuasi wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Margaret Thatcher, ni mwanasiasa wa mrengo wa kihafidhina wa kijamii.

Ni kiongozi wa chama tawala cha LDP, Takaichi amechaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa Japan baada ya kushinda kura ya uongozi katika bunge.

Baada ya ushindi huo, alitarajiwa kukutana na Mfalme Naruhito leo Jumanne (Oktoba 21, 2025), hatua inayothibitisha rasmi nafasi yake katika historia ya nchi hiyo.

Asili na historia ya Takaichi

Takaichi, mwenye umri wa miaka 64, alianza siasa miaka ya 1990 kama mwanachama wa chama cha LDP. Alizaliwa katika Jimbo la Nara, katikati mwa Japan, na alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Kobe.

Tofauti na wanasiasa wengi waandamizi wa LDP wanaotoka familia tajiri na waliopitia vyuo maarufu kama Chuo Kikuu cha Tokyo au Harvard Kennedy School, Takaichi anatoka katika mazingira ya kawaida.

Anajulikana zaidi kama mrithi wa kisiasa wa aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, hayati Shinzo Abe, ambaye alihudumia katika baraza lake la mawaziri mara kadhaa, na pia katika serikali ya Fumio Kishida.

Itikadi na misimamo yake ya kisiasa

Takaichi ni mfuasi mkubwa wa Margaret Thatcher, jambo lililomfanya kuitwa na vyombo vya habari ‘Iron Lady wa Japan’.

Katika kinyang’anyiro cha hivi karibuni cha uongozi, alitetea sera za kiuchumi zenye misingi ya “Abenomics” yaani mikakati ya kupanua matumizi ya serikali, kulegeza sera za kifedha, na mageuzi ya kimuundo.

Kwenye masuala ya kijamii kiongozi huyo ana msimamo mkali kuhusu uhamiaji, anaamini kuwa urithi wa kifalme bado unapaswa kupewa kipaumbele kwa wanaume.

Safari ya Takaichi kuelekea uongozi haikuwa rahisi. Atakuwa waziri mkuu wa nne wa Japan ndani ya miaka mitano.

LDP, licha ya kuwa chama tawala kwa muda mrefu, imepoteza wingi wa viti kwenye mabunge yote mawili katika miaka ya karibuni. Muungano wake wa zamani na chama cha Sanseito ulivunjika kutokana na migogoro kuhusu michango ya kampeni na rushwa.

Imeandikwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mitandao