Tanzania kutumia diplomasia ya uchumi, uwekezaji badala kutegemea misaada

Dar es Salaam. Tanzania inapanga kuvutia uwekezaji wa kati ya dola za Marekani bilioni 1 hadi 1.5 kutoka nchi za Nordic, pamoja na kuwasilisha miradi 17 ya kipaumbele.

Serikali imezindua mkakati wa ushirikiano wa Tanzania na nchi za Nordic unaolenga kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuhamasisha uwekezaji, badala ya utegemezi wa misaada.

Hayo yamebaishwa na Waziri wa Wizara hiyo Balozi Mahmoud Thabit Kombo alipokutana na mabalozi wa nchi hizo za Nordic ikiwemo Denmark na Sweden walioko nchini Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa maendeleo, uwekezaji na biashara endelevu.

Kikao hicho kimefanyika jijini Dar es Salaam ikiwa siku chache zimepita tangu kufanyika kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika na Nordic uliofanyika Victoria Falls, Zimbabwe Oktoba 2 na 3, 2025.

Akifafanua zaidi Waziri Kombo amesema Serikali imezindua mkakati huo wa ushirikiano unaolenga sekta tisa za kipaumbele, ikiwemo nishati jadidifu, miundombinu, elimu ya ufundi, uchumi wa buluu, viwanda, misitu na biashara kupitia mpango wa Aid for Trade.

“Tanzania inapanga kuvutia uwekezaji wa kati ya dola za Marekani bilioni 1 hadi 1.5 kutoka Nordic, pamoja na kuwasilisha miradi 17 ya kipaumbele inayotekelezwa kwa ushirikiano na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza).

“Hii ni kwa ajili ya kuendeleza teknolojia, ubunifu na ajira jumuishi. Pia nitoe wito kwa taasisi za kifedha za Nordic kama Norfund, Finnfund na Swedfund kushirikiana na Serikali kuanzisha mfuko wa pamoja wa ufadhili wa uwekezaji,” amesema.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kombo ameshukuru Nordic kwa uhusiano wa muda mrefu ulioanza tangu Tanzania ilipopata uhuru, akibainisha kuwa Tanzania imeendelea kunufaika na misaada na miradi ya sekta za elimu, nishati, afya, utawala bora na umeme vijijini.

Amesema mchango huo umejenga msingi wa uhusiano wa kuaminiana na ushirikiano wenye manufaa kwa wananchi.

Kwa upande wao, mabalozi wa nchi za Nordic wameeleza dhamira ya kuendeleza uhusiano na Tanzania kwa kuhamisha mkakati kutoka mfumo wa misaada kwenda katika ushirikiano wa usawa, unaolenga diplomasia ya kiuchumi huku wakisema historia ndefu ya urafiki kati ya pande hizo mbili imeweka msingi imara wa kukuza fursa mpya za biashara, uwekezaji na maendeleo ya pamoja.

Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlota Macias ameshukuru na kusifu ubunifu wa mawazo yaliyowasilishwa, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Sweden na Tanzania unaolenga maendeleo endelevu.

Amesema maeneo tisa ya kipaumbele yaliyotajwa na Tanzania yanaendana na vipaumbele vya Sweden, hasa katika nishati safi, teknolojia bunifu, na kusaidia viwanda vidogo.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mchakato wa kutoka utegemezi wa misaada kwenda kwenye uhusiano wa kibiashara (Aid-to-Trade Transition), huku akipongeza juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Jesper Kammersgaard, amesisitiza hatua hiyo inaonyesha dhamira ya dhati ya Tanzania katika kutekeleza mkakati mpya wa diplomasia ya kiuchumi.

Ameeleza nchi za Nordic zinathamini ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na zinalenga kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya pande zote.

Aidha, amesema nchi za Nordic sasa zinajikita zaidi kuwa washirika wa maendeleo badala ya kuwa wafadhili, na amesisitiza umuhimu wa kushirikiana katika masuala ya kimataifa kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mageuzi ya mfumo wa UN.