Dar es Salaam. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye ametoa wito kwa Serikali na wadau kuongeza uwekezaji na fursa katika elimu ya juu.
Amesema Taifa linahitaji elimu ya juu wenye nguvu kazi bunifu na uwezo wa kubadilisha uchumi wa kisasa.
Profesa Anangisye amesema licha ya hatua ambayo imepigwa hadi sasa kwenye elimu ya juu bado upo uhitaji wa kuongeza wigo zaidi ili kuongeza idadi ya wanaofikia elimu ya juu.
Profesa Anangisye alisema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na wahariri na waandishi wa vyombo kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
“Tunapozungumzia maendeleo endelevu, hatuwezi kuyaona bila kuwa na watu waliobobea kitaaluma. Dunia ya leo inahitaji wataalamu katika kila sekta sayansi, teknolojia, uchumi, kilimo, afya na utawala bora. Hivyo, ni jukumu letu kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata elimu ya juu yenye ubora.
“Elimu ya juu si kwa ajili ya kupata ajira tu, bali ni nyenzo ya kubadilisha fikra na kukuza jamii yenye uwezo wa kutatua matatizo yake. Tukiongeza fursa za elimu ya juu, tutakuwa tunawekeza moja kwa moja katika mustakabali wa taifa letu,”amesema Profesa Anangisye.
Hilo linakifanya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia mradi wa HEET kutekeleza mkakati wa kupanua wigo wa wanafunzi kwa miundombinu ya madarasa na vyumba vya maabara kwa kampasi kuu ya Mwalimu Nyerere, uboreshaji wa Kampasi ya Chuo cha Bahari Zanzibar na ujenzi wa kampasi mpya katika mikoa ya Lindi na Kagera.
Hatua hiyo inakwenda sambamba na uwekezaji katika mifumo ya Tehama na utengenezaji wa mitalaa inayoweza kutolewa kwa njia ya mtandao na kumfukia mwanafunzi popote duniani.
Profesa Anangisye amesema katika mradi huo, UDSM iimeimarisha miundombinu ya mtandao inayoweza kupokea na kusambaza mtandao kwa 10Mbps kutoka uwezo wa awali wa 1.5Mbps.
Mbali na hilo vimefungwa vifaa vya kisasa vya kufundishia kwenye kumbi za mihadhara vyenye uwezo wa jumla wa wanafunzi 8,000 kwa mara moja.
Profesa Anangisye amesema mradi huo pia umeandaa mifumo ya kisasa ya kufundisha kwa njia ya kidijitali yenye sifa za kutumiwa na wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
“Hadi sasa jumla ya masomo 1,000 yameingizwa kwenye mfumo. Kwa sasa wanafunzi 39,000 (wakiwemo 165 wenye mahitaji maalumu) na walimu 600 wameingizwa kwenye mfumo,”amesema.

Eneo lingine ambalo amelizungumzia Profesa Anangisye ni maboresho ya mitalaa, kupitia mradi huo UDSM, imefanyia mageuzi jumla ya mitalaa 250 kusudi iweze kuendana na soko la ajira.
Mmoja wa wanafunzi chuoni hapo, Joseph Mlay amesema kuna umuhimu wa kuoanisha mitalaa ya vyuo vikuu na mahitaji ya soko la ajira.
“Vijana wanapaswa kufundishwa stadi za karne ya 21 uhandisi wa kidijitali, akili bandia na ujasiriamali wa kisayansi. Bila kufanya hivyo, hata tukiongeza udahili, hatutakuwa tumejibu mahitaji ya uchumi wa kisasa,” amesema Mlay.
Naibu Mratibu wa HEET katika chuo hicho, Liberato Haule amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo 21 inayohusisha kumbi za mihadhara, karakana, studio, maabara na hosteli zitakazowezesha kuchukua wanafunzi 437.
Amesema chuo kinatekeleza mpango mahususi wa kukuza ushirikiano kati ya chuo na sekta binafsi katika ubunifu na biashara ya teknolojia.
Dk Haule amebainisha katika eneo hilo umewekwa mfumo na utaratibu unaoongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uendeshaji wa chuo.
“Tumeanzisha ofisi maalumu kwa ajili ya uhusiano na sekta binafsi na waajiri, pia tuna kamati malaumu zinazoshauri chuo masuala ya mitalaa, utafiti, ubunifu na huduma kwa jamii. Hadi sasa, kupitia kamati za ushauri za kitasnia, UDSM imesaini makubaliano ya mashirikiano na kampuni 24.
“Kupita makubaliano haya, tumeweza kupeleka wahitimu zaidi ya 100 kupata uzoefu wa kazi baada ya kuhitimu. Aidha wahadhiri 38 walipata uzoefu kwenye maeneo ya kazi. Yote haya yanachangia kuongeza ubora wa wahitimu wetu,” amesema Dk Haule.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema kuanzishwa kwa kampasi za Kagera na Lindi kumevunja mwiko wa kila anayetaka kusoma, lazima aje Dar es Salaam.
“Ifike wakati Watanzania tupende vitu vyetu, haya yaliyofanywa na UDSM ni makubwa, tusione shida kusifia na tusiishie kutafuta mabaya tu. Sisi kama wanahabari tunaahidi ushirikiano wa kuyatangaza mazuri yanayofanyika,” amesema Balile.