TUGHE YATOA RAI KWA WAFANYAKAZI KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU KWA KUCHAGUA VIONGOZI WATAKAOLINDA NA KUSIMAMIA MASLAHI YA WAFANYAKAZI

Na Mwandishi Wetu, KIBAHA PWANI

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimetoa rai kwa Wafanyakazi Nchini kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika Oktoba 29 kwa kuchagua Viongozi watakaosimamia na kulinda maslahi ya Wafanyakazi.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa TUGHE ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania ( TUCTA) Cde. Hery Mkunda alipokuwa Mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti na Makatibu wa Matawi ya TUGHE Mkoa wa Dar es salaam kilichofanyika leo Jumanne tarehe 21 Oktoba 2025 Kibaha Mkoani Pwani.

“Siku ya Uchaguzi tujitokeze kwenda kushiriki kwani ni haki yetu Kikatiba na lazima tuhakikishe tunaitumia vizuri haki hii kwa kuchagua Viongozi watakaosimamia na kulinda maslahi ya Wafanyakazi wote wa Tanzania” Alisisitiza Cde. Mkunda

Katika hatua nyingine Cde. Mkunda ameendelea kuishukuru Serikali ya Awamu ya 6 inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushughulikia changamoto mbalimbali za Watumishi ikiwemo Upandishwaji wa Vyeo na Madaraja kwa Watumishi wa Umma, ambao ulikuwa umesitishwa tangu Mwaka 2016, Ongezeko la Kima cha chini cha Mshahara kwa Watumishi wa Sekta Binafsi na Umma pia ongezeko la Siku za Likizo ya Uzazi kwa Wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti.

Aidha katika hatua nyingine Katibu Mkuu wa TUGHE ametumia Kikao kazi hicho kutoa rai kwa Viongozi wote wa Matawi ya TUGHE Nchi nzima kuhakikisha wanafuata matakwa ya Katiba ya Chama kwa kuhakikisha Wanafanya Vikao vya Matawi kama inavyoelekeza.

“ Kwa taarifa tulizonazo ni kuwa baadhi ya Matawi yamekuwa hayafanyi Vikao vya Matawi yaani Mkutano Mkuu wa Tawi pamoja na Kikao cha Halmashauri ya Tawi hivyo kupelekea kuwanyima wanachama fursa ya kupata taarifa muhimu kuhusu sekta yao ya kazi pamoja na kukosa fursa ya kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali yanayohusu maslahi yao hivyo nitoe rai kwa Viongozi wote wa Matawi kutekeleza takwa hili la kikatiba ya Chama chetu kama inavyotuelekeza”

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dar es salaam Cde. Brendan Maro alimshukuru Katibu Mkuu kwa kuja kufungua Kikao Kazi hicho ambapo pamoja na mambo mengine kinakusudia kuwakutanisha Viongozi wa Matawi ya TUGHE kutoka Mkoa huo ili waweze kubadilishana uzoefu katika usimamizi na uendeshaji wa shughuli za Chama Matawini katika maeneo yao ya Kazi.