Vaibu Yanga Mzize akirejea kupiga mzigo 

KULE Malawi wiki iliyopita, Yanga ilisafiri ikiwa na mshambuliaji wake hatari, Clement Mzize, lakini hakucheza dhidi ya Silver Strikers katika mechi ya awali ya mkondo wa pili wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mzize alisafiri akiwa na kikosi hicho ambacho kilipoteza ugenini kwa bao 1-0, na kilichoelezwa ni kwamba nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania alikosekana kutokana na kuwa katika kipindi cha mpito akitokea katika majeraha yaliyomuweka nje kwa takriban mwezi mmoja.

Lakini unaposoma hapa ni kwamba kikosi hicho kimepata nguvu zaidi baada ya Daktari wa Yanga, Moses Etutu kuthibitisha kwamba mshambuliaji huyo yupo tayari kucheza mechi ya Jumamosi, kwani hivi sasa yupo fiti kwa asilimia mia.

Itakumbukwa kwamba wakati Yanga ikiwa Malawi mchezaji huyo alionekana akifanya mazoezi na wenzake kabla ya kurejea hapa nchini.

MZI 01

Mzize ambaye alikuwa kinara wa ufungaji kwa wachezaji wazawa ndani ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga mabao 14, huku akimaliza wa pili nyuma ya Jean Charles Ahoua wa Simba aliyefunga 16, alipata majeraha wakati Yanga ikiichapa Wiliete SC ya Angola mabao 3-0 kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa Angola.

Etutu ameliambia Mwanaspoti suala la mshambuliaji huyo kucheza, wameliacha kwa kocha huku akisisitiza kuwa kwenye hali ya utimamu akiwa ameanza mazoezi sambamba na wachezaji wengine.

“Kwa sasa yupo salama kwa asilimia 80, ni mzima, mechi ijayo ni ruksa kwake kucheza kama kocha atakuwa na utayari wa kumtumia kwani anaendelea vizuri, hadi mwishoni mwa wiki iliyoisha utimamu wake ulikuwa tayari, naamini kocha sasa atakuwa na program ya kumpa ili arejee haraka kwenye ushindani.

MZI 02

“Mzize ameweza kufuata ratiba yote aliyopewa wakati wa mapumziko yake ya wiki tatu, hivyo hakutakuwa na muda wa kumpa program nyingine ya kufuata ndio maana ameingia moja kwa moja kwenye kikosi kwa ajili ya mazoezi, nafikiri suala la kucheza Jumamosi lipo chini ya kocha, sisi chini yetu tumempima na kubaini kuwa yupo tayari,” amesema Etutu.