WAKATI baadhi ya makocha wa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), wakitoa malalamiko kwa baadhi ya waamuzi kutotenda haki huku wakiziomba mamlaka kuwachukulia hatua, Chama cha Waamuzi Zanzibar kimesema malipo yanaweza kuwa chanzo kikubwa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi Zanzibar, Waziri Sheha, baadhi ya viongozi wa klabu wanatumika kuwarubuni waamuzi kwa kuwaahidi fedha nyingi kutokana na malipo yao kuwa kati ya Sh20,000 hadi Sh30,000 kwa mechi moja.
“Ukweli changamoto kubwa ni viongozi wa klabu ndio wanaowaharibu waamuzi kwa kuwarubuni, kabla ya mechi kiongozi anamtafuta na kumuahidi atamwezesha. Kwa hali ya kawaida mwamuzi analipwa Sh20,000 hadi Sh30,000 kwa mechi moja, lakini huku ameahidiwa Sh100,000, hivyo kama binadamu hataiacha fedha hiyo,” amesema Sheha.
Amesema changamoto hiyo ndio sababu kubwa inayofanya kutokea kwa uamuzi tata wakati wa mechi ingawa chama hicho kinawataka waamuzi kuchezesha kwa haki kwani huo ni mchezo wa wazi na kila shabiki anaona.
Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa viongozi kuacha tabia hizo ili kulikuza soka la Zanzibar na waamuzi kufuata sheria 17 za soka.
Baadhi ya makocha waliozungumza na Mwanaspoti, wamesema waamuzi wanaochezesha chini ya kiwango wamekuwa sababu ya kuichafua ligi hiyo, jambo ambalo linaua nguvu na hamasa Zanzibar.
Mzee Ali Abdallah ambaye ni Kocha Msaidizi wa Chipukizi amesema, “Tunazitayarisha timu kuwa na ushindani, jambo la kusikitisha waamuzi wanauharibu mchezo kwa kukubali bao la kuotea na kumwachia mchezaji akiwa nafasi hiyo bila ya kuitafsiri sheria namba 11 ya mpira wa miguu.”
Kocha Mkuu Fufuni, Suleiman Mohamed amesema endapo waamuzi wakichezesha inavyostahili Ligi Kuu Zanzibar itakuwa na ushindani mkubwa.
Katika kukabiliana na changamoto hizo za waamuzi, Bodi ya Ligi Zanzibar, tayari imemwondoa mwamuzi Washington Benard katika ratiba kwa mizunguko mitano baada ya kushindwa kuzitafsiri na kuzisimamia sheria 17 za mpira wa miguu katika mechi iliyozikutanisha JKU na KVZ.
Katika mechi hiyo ya Oktoba Mosi, 2025 ya sare ya mabao 2-2, mwamuzi huyo anatuhumiwa kukataa bao la JKU ikidaiwa mfungaji aliotea. Adhabu hiyo imetoka kwa kuzingatia kanuni ya 3 sura ya 27 ya mashindano.