Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula (kulia) akisalimiana na wananchi wa kata ya Iparamasa.
….,……,…..
CHATO
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chato kusini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Paschal Lutandula, amewahakikishia utajiri wachimbaji wadogo wa dhahabu iwapo atachaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo hilo.
Ni kutokana na mazingira mazuri yaliyo wekwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi katika kuboresha maisha ya kila mtanzania.
Lutandula akiwa katika mkutano wa kampeni za CCM kwenye Kijiji cha Iparamasa kata ya Iparamasa ameonyesha matumaini makubwa kwa wachimbaji wadogo kwa madai hapendi kuona wakiendelea na uchimbaji usio na tija.
“Niwahakikishie wananchi wa Iparamasa, Oktoba 29 mkinichagua mimi kuwa Mbunge, Dkt Samia kuwa Rais wa Tanzania pamoja na Diwani Peter Mbasa kuwa mwakilishi wenu, mtanufaika na shughuli zenu za uchimbaji madini”,
“Wachimbaji madini mtachimba kwa amani bila wasiwasi wowote, nitasimama na ninyi wakati wote ili kuhakikisha mnakuwa matajiri, na Dkt. Samia ameshaahidi kununua ndege kwaajili ya kuchunguza maeneo yenye Madini ili mchimbe kwa uhakika na mfanikiwe kutajirika” amesema Lutandula.
Pia ameahidi kuziboresha barabara za kata hiyo kwa kununua mitambo ya kutengeneza miundombinu hiyo ili kuchochea uchumi wa wananchi wakiwemo wakulima.
Kadhalika amesema nia yake ni moja na ya dhati kuwatumikia wananchi hao na kwamba hatojikweza kutokana na nafasi atakayoipata huku akiwataka kuendelea kumuombea dua na sala katika azma yake ya utumishi wa umma.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata hiyo, Peter Mbasa, akawataka wananchi hao kumchagua Dkt. Samia, kwa kura nyingi ili ashinde kwa kishindo, Lutandula pamoja na yeye ili waharakishe maendeleo yanayo kusudiwa.
Amewakumbusha kutunza vizuri kadi zao za kupigia kura ili Oktoba 29 mwaka huu watimize haki yao ya msingi kwa kuwachagua viongozi wanaofaa kwa maslahi mapana ya Kata hiyo pamoja na Tanzania kwa ujumla.
Mwisho