ALIYEKUWA Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo( CHADEMA) kwa miaka 15 Ezekia Wenye amesema waliokwamisha mchakato wa kupata Katiba Mpya ni vyama vya upinzani.
Wenje ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya ziwa inayojumuisha mikoa ya Mwanza,Geita na Kagera ametoa kauli hiyo leo Oktoba 21,2025 wakati wa mkutano wa Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan uliofanyika Viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.
Akifafanua zaidi katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Kinondoni na Ubungo,Wenje amesema wapo wanaosema Serikali ya CCM imekwamisha kupatikana kwa Katiba Mpya lakini ukweli waliokwamisha kupatikana kwa Katiba Mpya ni wqpinzani.
“ Wapinzani wa nchi hii ndio tulikimbia Bunge la Katiba ,tuliotoka nje na ukweli wapinzani na mimi wakati huo nilikuwa huko .Ninawaambia Watanzania wapinzani waliokwamisha Katiba Mpya,”amesema Wenje ambaye kwa sasa ni mwanachama wa CCM.
Katika mikutano ya kampeni ya Mgombea urais Dk.Samia Suluhu Hassan,Wenje amekuwa akitoa siri za vyama vya upinzani na hasa CHADEMA ambako yeye amekuwa huko kwa muda mrefu.
Pia amesema kuwa hata CHADEMA kutoshiriki Uchaguzi Mkuu mwaka huu hawajazuiwa na Serikali bali wenyewe ndio wameamua kutoshiriki uchaguzi huo na yeye sababu ambazo zimewafanya kukimbia uchaguzi mkuu anazijua.
“Nilikuwa kule hivyo najua sababu za kutoshiriki uchaguzi na siku wakileta Pang’aa nitasema kwasababu gani wameweka mpira kwapani na kutoshiriki uchaguzi mkuu.”
Wakati huo huo Wenje amesema historia ya Rais Dk.Samia alipokuwa akielezea kwenda Mkoa wa Rukwa kwa mara ya kwanza akiwa mfanyakazi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali aliyekwenda kufanya utafiti alizungumzia alivyokwama barabarani .Jinsi alivyokuwa akienda katika duka la Mpenda aliyekuwa Sumbawanga mkoani Rukwa.
“Katika historia ya Dk.Samia alipoenda Mkoa wa Rukwa.Nilichojifunza hatma ya mwanadamu iko kwa Mungu mwenyewe,yule Mpemba ambaye Dk.Samia anakwenda dukani hakuwa anajua kama iko siku Dk.Samia atakuwa Rais.”
Ameongeza kwamba:”Hatma ya mwanadamu inaamriwa na Mungu hivyo mtanzania usikate tamaa hata kama unakula ugali na dagaa amini katika Mungu huenda katika familia hiyo anaandaliwa Samia mwingine.”