ADC yaahid kusomesha wanafunzi kompyuta kuanzia maandalizi hadi chuo kikuu

Pemba. Mgombea urais  wa Zanzibar kupitia chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed, amesema akichaguliwa na wananchi kuiongoza nchi, ataanzisha utaratibu wa kusomea kompyuta kuanzia maandalizi hadi chuo kikuu ili kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 22, 2025, alipozungumza na wananchi na wanachama wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Masota, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Mgombea huyo amesema katika kufanikisha utaratibu huo ataanzisha kiwanda maalumu cha kutengenezea kompyuta, kitakachowapa fursa vijana kuendana na mifumo ya teknolojia.

Amesema utaratibu huo utawasaidia wanafunzi katika masuala ya ufundishaji pamoja na kupunguza mzigo wa vitabu wanapokwenda shuleni.

Aidha, kuwepo kwa kiwanda hicho kutaongeza uzalishaji wa vifaa vya kielektroniki vitakavyowasaidia wanafunzi kujifunza matumizi ya mifumo ya teknolojia.

“Mtakaponichagua kuwa Rais wenu, nitajenga kiwanda cha kompyuta kitakachozalisha vifaa vya kielektroniki vitakavyosaidia wanafunzi kuanzia maandalizi hadi chuo kikuu kujifunza na kuendana na mifumo ya teknolojia,” amesema.

Mgombea huyo ameongeza kuwa kiwanda hicho pia kitatumika kupunguza gharama za kununua vifaa kutoka nje ya Zanzibar na kuimarisha uchumi wa eneo hilo kwa kuendana na mifumo ya kisasa ya teknolojia.

Kwa upande wake, meneja wa kampeni wa chama hicho, Yussuf Salim Khamis, amesema chama kimejipanga kuzingatia maslahi ya wananchi kwa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kupata mitaji itakayokuza biashara zao.

“Sisi chama chetu kinaangalia zaidi maslahi ya wananchi, tutawawezesha wajasiriamali kwa kuwapatia mitaji ili kuinua kipato chao,” amesema Khamis.

Awali, mgombea wa uwakilishi Jimbo la Kojani kupitia tiketi ya ADC, Mbarouk Omar Mbarouk, amesema iwapo wananchi watamchagua kuwa kiongozi wao, ataimarisha sekta ya kilimo kwa kuwapatia wakulima pembejeo na matrekta ili kuachana na kilimo cha mikono, jambo litakaloongeza uzalishaji wa mavuno, hasa ya mpunga.