Anayedai kutumwa na Mungu kesi ya Lissu alivyoondolewa mahakamani

Dar es Salaam. Unaweza kudhani ni tamthilia ya OttoMan inarekodiwa mahakamani, lah hashaa! bali ni tukio halisi baada ya mtu mmoja ambaye alipaza sauti akiomba kutoka juu eneo wanalokaa wasikilizaji wa kesi katika Mahakama ya wazi namba moja iliyopo  Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Mtu huyo aliyevalia shati jeupe, tai nyeusi na suruali rangi nyeusi  ambaye alikuwa amekaa eneo hilo lililopo kwa juu, alileta taharuki mahakamani hapo wakati kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu ikisikilizwa.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano Oktoba 22, 2025 saa 3:30   asubuhi, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi na wakati Jaji Dustan Nduguru akianza kusoma uamuzi huo, lakini ghafla mtu huyo ambaye hajafahamika jina lake alianza kuimba Yesu wangu, Yesu wangu niokoe.

Mwanaume huyo awali alisikika kama akipiga maombi na baadaye alipaza sauti juu huku akisema kuwa anataka majaji wamsikilize kwa sababu yeye yupo mahakamani hapo tangu jana na ametumwa na Mungu

“Nipo hapa mahakamani tangu jana waheshimiwa hakimu, jaji, naomba mnisikilize maana nimetumwa na Mungu.”

Hali hiyo ilipelekea Jaji Nduguru kutangaza kuwa kesi inaendelea na watu wasipige picha wala kusimama kugeuka nyumba kuangalia juu ya ukumbi huo ambapo jamaa huyo alikuwa akisikika akiongea.

Hali hiyo ilidumu  kwa dakika nne na kisha askari Polisi pamoja na askari Magereza waliokuwepo ndani ya Mahakama hiyo,  walipanda juu na kwenda kumchukua mwanaume huyo huku akigalagala chini na kufanikiwa kutolewa na kisha kesi hiyo kuendelea.

Watu wote ndani ya ukumbi wa mahakama wakiwa wametulia, mshtakiwa Lissu akaletwa ukumbini na askari Magereza kama ilivyo utaratibu, kisha baada ya muda kidogo jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru, wakifuatana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde nao pia waliingia mahakamani hapo.

Punde tu majaji walipoketi kwenye nafasi zao kwa ajili ya kusoma uamuzi, ghafla ilisikika sauti kutoka eneo la juu la ukumbi wa mahakama ikisema Waheshimiwa Majaji wa Mahakama hii naomba mnisikilize nimetumwa na Mungu”  huku akiendelea kuongea ndipo askari walipopanda juu kwa haraka na kwenda kumtoa mtu huyo.

Hata hivyo mtu huyo alionekana kugoma kutoka akidai anataka kuongea. Askari walilazimika kumbeba kwa nguvu na kumtoa nje huku akiendelea kusema: Yesu nisaidie…yesu nisaidie”

Mwanaume huyo alitolewa nje ya mahakama akiwa ameshikwa mikono na miguu  chini ya ulinzi wa askari kanzu.

Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wafuasi na wanachama wa chama hichi waliokaa juu walionekana kushangalia maneno aliyokuwa akiyatoa mtu huyo, huku watu wengine ambao sio wafuasi wa chama hicho wakipigwa na butwa kuona tukio hilo likitokea wakati kesi ikiendelea mahakamani.