Dk Nchimbi ataja mambo matatu yanayombeba Samia

Kyela. Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ametaja mambo matatu yanayombeba Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu utakaofanyika siku saba zijazo.

Amesema kazi kubwa iliyofanywa kwa kipindi cha miaka minne na nusu ya utawala wa Rais Samia pamoja na mambo mengine, imewaheshimisha wanawake na chama hicho ndani na nje ya nchi.

Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumatano, Oktoba 22, 2025 katika mkutano wa kampeni, uliofanyika Uwanja wa mpira wa Mwakangale, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya.

Ni mikutano ya lala salama za kampeni kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 ambapo Watanzania milioni 37.6 ndiyo walioshika hatima ya nani awe diwani, mbunge na Rais.

Vyama 18 kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu vinashiriki uchaguzi huo ambao kuna wagombea 17 wa urais, wakiwania kuingia Ikulu kuwatumikia Watanzania kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imekwisha eleza maandalizi ya vifaa tayati vimefika kwenye halmashauri zote Tanzania Bara na Zanzibar yamekamilika.

Katikati ya hayo, Dk Nchimbi kwenye mkutano huo wa Kyela ameyataja mambo matatu yanayomfanya Samia kumbeba kwenye mbio za urais dhidi ya washindani wenzake 16 wa urais ambao ni kilimo, afya na elimu.

“Rais Samia ameyafanyia kazi vizuri mpaka dunia inashangaa,” amesema Dk Nchimbi.

Amesema katika eneo la kilimo, Rais Samia ameleta mageuzi makubwa ikiwemo kuipandisha bajeti ya kilimo ya maendeleo zaidi ya mara sita:”Wakati Rais Samia anaingia madarakani kulikuwa na miradi mitatu, leo tunavyoongea ipo miradi 730.”

“Uzalishaji wa mazao ya chakula umepanda kutoka tani laki tatu na tisa mpaka zaidi ya tani milioni 1.2,” amesema.

Jambo la pili ni kwenye sekta ya afya ambapo Dk Nchimbi amesema Rais Samia amefanya mabadiliko makubwa ambayo: “Yametupa heshima sana. Wana CCM na Watanzania kwenye hospitali za wilaya.”

“Zipo baadhi ya Halmashauri katika nchi yetu zilikuwa hazina hospitali za Wilaya ndani ya miaka minne na nusu, ujenzi wa hospitali mpya 109. Lakini vilevile ndani ya miaka minne na moja, Rais Samia amewezesha ujenzi wa vituo vipya vya afya 667 nchi nzima, ujenzi wa zahanati mpya 2894,” amesema.

Jambo la tatu ni elimu, Dk Nchimbi amesema mageuzi makubwa yamefanyika kujenga shule mpya za msingi, madarasa, maabara na za sekondari ikiwemo maalumu kwa wasichana kila mkoa kujengwa moja.

Katika mitano ijayo Kyela, Dk Nchimbi amesema wanakwenda kuiboresha zaidi hospitali ya Wilaya kwa kuiongezea majengo, vifaatiba pamoja na wataalam kwa maana madaktari na wauguzi.

Amesema wanakwenda kujenga vituo vipya vya afya vinne na zahanati mpya saba na nyumba 11 za watumishi pamoja na ujenzi wa chuo cha uguzi Kyela.

Skimu za umwagiliaji, miradi ya maji, ujenzi wa barabara, soko la kimkakati la mazao ni miongoni mwa ahadi ambazo Dk Nchimbi amezitoa kwa wananchi na kuwaomba wakichague chama hicho, Oktoba 29, 2025.

Nimezaliwa Mbeya, msiniangushe

Safari yake ya maisha hapa duniani, Dk Nchimbi aliianza Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya. Ndipo alipozaliwa kipindi hicho, baba yake, John Nchimbi akifanya kazi mkoani humo. Kiasiki, yeye ni mgoni wa Songea, Mkoa wa Ruvuma.

“Mimi nimezaliwa Mbeya Mjini na huu ni moja ya mkoa wangu wa nyumbani,” amesema Dk Nchimbi huku akishangiliwa.

Hotuba yake ikikatishwa mara kadhaa na shangwe akasema: “Sasa Oktoba 29 msiniangushe, tumchague Mama Samia kwa kura nyingi huku mkijua kabisa amemchukua (Dk Nchimbi) mzaliwa wa Mbeya kuwa msaidizi wake na nchi nzima wanajua nimezaliwa Mbeya, hafu atokee mtu tu apige kura ya hapana.”

Amesema ikiwa atawiwa kuwania ubunge basi majimbo matatu yanahusika la Mbeya Mjini, Songea Mjini na Nyasa ya Ruvuma. Amewahi kuwa mbunge wa Songea Mjini 2005-2015.

Dk Nchimbi amesema, hata uongozi alianzia Mbeya Mjini kama Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) na alipotaka kuwania uenyekiti wa umoja huo mkoa wa Mbeya alishindwa.

Alicholisema Mwamengo, Qwihaya

Mgombea ubunge wa Kyela, Baraka Mwamengo amesema mambo mengi yamefanyika wilayani humo kwenye kila sekta lakini kuna changamoto alizoziita ndogondogo za maji, barabara na za kilimo akiomba zitafutiwe ufumbuzi.

Mwamengo anayewania jimbo hilo awamu ya kwanza amesema zao la kokoa:”Tunaomba uwepo wa kiwanda hapa ili tuwe na uhakika wa bei.”

Pia, amesema Kyela kwa sasa ni Mamlaka ya Mji mdogo na sasa wananchi wameongezeka hivyo ameomba wapate halmashauri kamili.

Mratibu wa kampeni za chama hicho, mikoa ya nyanda za juu Kusini, Leornad Qwihaya amesema hakuna ubishi kwamba chama hicho kimekwisha kushinda udiwani, ubunge na urais:”Lakini tumeshinda shindaje?, Hilo ndilo swali ambalo tunataka kujiuliza.”

“Tunataka tuyaone kwa sababu mpira ni dakika tisini. katika jimbo la Kyela tuna wapiga kura 163,061, lakini tuna wanachama wa Chama cha Mapinduzi 58,630,  ndugu zangu, pamoja na kuwa tumeshinda lakini tunashinda kwa kura zipi?.”

Qwihaya amesema wameongea na madiwani na watendaji pamoja na mabalozi:”Lakini nataka niwasisitize wanachama wa Chama cha Mapinduzi katika kura 163,061 tuna wanachama karibia elfu sitini maana yake kila mwanachama akienda na mwingine tumeshinda kwa kishindo.”