Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza vyombo vya ulinzi na usalama ndani ya Taifa hili vimejipanga vema na vina uwezo wa kutosha na nchi iko salama wakati wote iwe wakati wa uchaguzi iwe hakuna uchaguzi
Hivyo ametoa mwito kwa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 mwaka huu kupiga kura kwani nchi ipo salama wakati wote.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajia kufabya Oktoba 29 mwaka huu ,Dk.Samia amewahakikishi Watanzania nchi iko salama.
Dk. Samia amesisitiza kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vipo makini wakati wote kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa salama.
“Niliongea jana nataka niongee tena leo , vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ndani ya taifa hili vimejipanga vyema, tumevijengea uwezo wa kutosha.
“Tupo salama wakati wote iwe wakati wa uchaguzi, iwe hakuna uchaguzi tupo salama wakati wowote. Hivi vimatishio vidogo wanavyovifanya kama mnawaelewa nendeni mkawaulize.Niwatoe hofu wananchi, nendeni mkajitokeze mkapigekura, tupo salama wakati wote.”
Katika hatua nyingine Dk.Samia Suluhu Hassan amewasisitiza wananchi katika uchaguzi mkuu mwaka huu wachague Chama Cha Mapinduzi(CCM) na wagombea wake wote wa udiwani,wabunge pamoja na Rais ambaye ni yeye.
”Nendeni mkachague CCM,msichanganye rangi,tuchagueni wagombea wa CCM tukaendelee kufanya kazi ya kuleta maendeleo tuendeleze utu wa Mtanzania.”