Songwe. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara, amesema bado Taifa halijaipa kipaumbele suala la elimu, akieleza akichaguliwa atajikita kuweka usawa kwa walimu na wanafunzi.
Pia mgombea huyo ametumia mkutano wake katika Mji wa Mlowo, mkoani Songwe, kuwaomba Watanzania kuwaombea wanafunzi wa darasa la nne kumaliza salama mitihani yao waliyoanza leo Oktoba 22, 2025.
Akizungumza katika mkutano huo, Kyara amesema bado mazingira ya shule nyingi nchini yana changamoto kwa kutokuwa na walimu wa kutosha, akiahidi kuwa Serikali ya SAU itaweka uwiano baina ya walimu na wanafunzi.
Amesema ilani ya chama hicho kitaweka utaratibu wa kila shule kuwa na mwalimu mmoja kwa wanafunzi 20–29, tofauti na ilivyo sasa ambapo mwalimu anafundisha wanafunzi 53, hali ambayo haimpi mafanikio makubwa kwa makundi hayo.
“Tunajua mwalimu akiwa na wanafunzi wachache ataweza kujua changamoto zao, kuwafundisha vizuri, na mwisho tutapata wajenzi wazuri wa Taifa kwa kizazi cha baadaye.
“Ili kufikia malengo hayo, SAU tutatoa ajira za kutosha kwa walimu ili kuweka uwiano wa wanafunzi 20–29 kwa mwalimu mmoja. Tumejipanga kuwahudumia vyema wananchi,” amesema Kyara.
Kyara ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya sasa kitaifa na kimataifa, inahitajika Katiba mpya, na kuwa iwapo chama hicho kitashinda, katiba hiyo inapatikana ndani ya wiki 40 bila kujali mchakato.

Amesema jambo lingine ni kukabiliana na rushwa nchini, akieleza kuwa kwa sasa inahitaji kiongozi anayefuata mabadiliko, akiahidi ataongoza nchi kwa hofu ya Mungu.
“Tunajua rushwa ni adui wa haki, tunahitaji nchi isiyo na rushwa, na mimi niwaahidi kuongoza nchi kwa hofu ya Mungu, tukitanguliza maslahi ya nchi. Ndiyo maana leo nimewafuata mlipo ili niweze kuona kero zenu,” amesema Kyara.
Mwenezi wa chama hicho Taifa, Shaban Kirita, amesema wananchi hawana budi kumchagua Kyara, ambaye ataweza kumaliza kero zinazowakabili, ikiwamo michango ya shule.
Amesema kumekuwa na utitiri wa kodi kwa wananchi, pamoja na kutekeleza ajira kwa vijana, tatizo limekuwa kubwa na kuwalazimisha wasomi kuishia kuendesha bodaboda.
“Wafanyabiashara ndogondogo mnajitahidi kusomesha watoto wenu kwa gharama na michango mingi, lakini wanapomaliza masomo hawapati ajira, na badala yake wanabanana nyumbani na mitaani.
“Sasa basi, suluhisho lenu ni Kyara wa SAU, ambaye atamaliza changamoto zote na kuleta usawa na haki kwa kila Mtanzania. Tumpe kura za ndiyo Oktoba 29,” amesema Kirita.
Mmoja wa wananchi katika Mji wa Mlowo, Jesca Mwashinga, amesema viongozi wanaofika kwa wananchi wanaonesha nia ya kuongoza nchi, akimshukuru mgombea huyo kuwatembelea na kusikia mahitaji yao.
“Siyo wote wagombea wamekuja hapa Mlowo, baadhi wamepita barabarani na wengine wameishia mikoa ya jirani, lakini huyu ametufikia Mlowo, tunamuombea,” amesema Jesca.