Mahakama ilivyokubaliana na Lissu video ya uhaini

‎‎Dar es Salaam: Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ambaye anakabiliwa na kesi ya uhaini, ameibwaga Jamhuri mahakamani katika pingamizi la upokewaji wa flash disk na memory card zenye video inayomuonyesha akitamka maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini.

Lissu ameshinda pingamizi hilo baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam inayosikiliza kesi hiyo kukubaliana na sababu yake moja kati ya nne za pingamizi hilo, kukataa kuvipokea vihifadhi data hivyo vyenye video hiyo.

Video hiyo ndio inamuonesha Lissu akitoa hotuba inayodaiwa kuwa na maudhui (maneno) ya uhaini, katika mkutano wake na waliokuwa watia nia kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao.

Sababu hiyo pekee ambayo imetosha mahakama kukataliwa kwa vielelezo hivyo ni kwamba shahidi wa Jamhuri aliyeomba kuziwasilisha hana mamlaka ya kisheria kwa kuwa hana sifa za kuwasilisha vielelezo hivyo.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano, Oktoba 22, 2025 na jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Katika kesi hiyo namba 19605 ya mwaka 2025, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha maneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa Jamhuri, ambapo mpaka sasa shahidi wa tatu wa Jamhuri anaendelea kutoa ushahidi wake.

Shahidi huyo wa tatu ni Mkaguzi wa Jeshi Polisi, Samweli Kaaya (39), Mtaalamu wa picha, kutoka kitengo cha Picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai. Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.

Katika ushahidi wake wa msingi alieleza kuwa Aprili 8, 2025 alipokea flash disk na memory card zenye video ya Lissu yenye maudhui yanayodaiwa kuwa ya uhaini,  kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Dar es Salaam kuchunguza  uhalisia wake.

Shahidi huyo  aliieleza Mahakama kuwa katika uchunguzi wake alibaini kuwa video hiyo ni halisi na haina pandikizi, Ijumaa iliyopita, Oktoba 17,  2025 aliiomba Mahakama ivipokee flash na kadi hiyo  picha hizo (video) ziwe kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Hata hivyo Lissu alipinga kupokewa kwa vihifadhi data hivyo vyenye video yake kuwa vielelezo vya ushahidi wa upande wa Jamhuri akibainisha sababu nne.

Lissu   alizitolea ufafanuzi wa kina katika mizania ya kisheria na msimamo wa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa mashauri mbalimbali  kuhusiana na hoja hizo.

Jamhuri pia katika majibu yake kupitia jopo la waendesha mashtaka, mawakili wa Serikali lilipinga vikali hoja hizo huku wakitoa ufafanuzi wa kina kukinza na hoja za Lissu, huku wakirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika mashauri mbalimbali kuishawishi Mahakama ikibaliane nao.

Hata hivyo Mahakama katika uamuzi wake leo, imejielekeza katika sababu moja pekee ambayo imetosha kukataliwa kupokewa kwa vihifadhi data hivyo kuwa vielelezo vya ushahidi wa upande wa mashtaka.

Katika orodha ya sababu hizo ilikuwa ya tatu, Lissu alidai kuwa shahidi huyo hana ustahili wa kisheria (incompetent) kuwasilisha vihifadhi data hivyo vyenye picha jongefu (video).

Alifafanua kuwa shahidi huyo si mtaalamu aliyeteuliwa na  mamlaka husika na kutangaza katika Gazeti la Serikali kama kifungu cha 216(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Urekebu wa Mwaka 2023.

Alibainisha kuwa kwa mujibu wa kifungu hicho, mtaalamu wa aina hiyo huteuliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kutangazwa katika Gazeti la Serikali.

Pia Lissu alidai kuwa shahidi huyo ameteuliwa kuwa mtaalamu wa picha za mnato na si mtaalamu wa picha jongefu na kwamba kwa kuwa vielelezo anavyokusudia kuziwasilisha vina picha jongefu basi shahidi huyo hana mamlaka ya kuziwasilisha.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga katika hoja hiyo alidai kuwa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa mashauri mbalimbali imetoa sifa ambazo mahakama inapaswa kuziangalia kabla ya kupokea ushahidi huo, ambazo ni uhusiano na kesi umuhimu na ustahilifu kisheria.

“Tunasema shahidi wetu pamoja na vielelezo hivi anakidhi matakwa ya kanuni kwa kuwa kielelezo kinachotakiwa kutolewa na shahidi anayehusika anastahili,” alisema Wakili Katuga.

Alisisitiza kuwa anastahili kwani kwanza ameieleza mahakama kuwa ndiye  aliyefanyia kazi vielelezo hivyo, pili ameeleza utaalamu.

Akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa mashauri mbalimbali amesema kuwa ustahilifu wa shahidi  ni kuwa na ufahamu wa kitu husika kama vile mmiliki,  mtunzaji au aliyekifanyia kazi.

Alisema kuwa shahidi katika ushahidi wake alieleza kuwa mtaalamu wa picha za mnato na jongefu na kwamba ametangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 516 la mwaka 2022 na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu kuwa mchunguzi wa picha na  kutoa taarifa.

Mahakama katika uamuzi wake uliosomwa na Jaji Ndunguru imekubaliana na hoja ya Lissu.

Jaji Ndunguru amesema Mahakama imefuatilia na kuchunguza kwa umakini hoja za pande zote imejiridhisha kuwa shahidi huyo hana mamlaka ya kuwasilisha vielelezo vya aina hiyo (video).

Jaji Ndunguru amesema kuwa shahidi huyo ni miongoni mwa wataalamu walioteuliwa na DPP kuwa mtaalamu wa picha na kutangaza kwenye G745/2022 Desemba 16, 2022.

Amesema kuwa katika aya ya pili ya Gazeti hilo walioteuliwa ni wataalamu wa uchunguzi wa picha kwa madhumuni ya kutoa taarifa kama ushahidi kwenye kesi ya jinai.

Jaji Ndunguru amesema kuwa kwa mujibu wa  kifungu cha 216(1) cha CPA, kinachompa mamlaka DPP kuteua na kutanga za wataalamu hao inazungumzia shahidi kuandaa picha zinazozalishwa kutoka kwenye filimu.

Hivyo amesema kuwa GN Namba 745 iliyomtangaza shahidi wa  tatu kifungu cha 216(1) kinazungumzia mtaalamu wa picha za mnato.

Hata hivyo Jaji Ndunguru amesema kuwa shahidi alichokiomba kuwasilisha mahakamani ni vibebeo vya picha mjongeo vyenye picha mjongeo katika mfumo wa kidijitali.

Amesema kuwa ingawa upande wa mashtaka ulijitahidi kuishawishi Mahakama kuwa picha zinazozungumzia hapo ni pamoja na picha mnato na video, lakini mahakama haikukubaliana na hoja hiyo.

Amefafanua kuwa kifungu cha 216(1) hajazungumzia video na kwamba vitu hivyo viwili (picha mnato na video) vina sifa tofauti na    mahakama imeona kwamba hiyo video si picha ambazo zimetokana na filimu.

Hivyo amesema kuwa mahakama imeona kuwa shahidi huyu asingeweza kuwasilisha vitu hivyo kwanza kwa mujibu wa uteuzi wake na pili hivyo vifungashio na vilivyomo.

Amesema kuwa mahakama inaona kwamba mtaalamu wa picha mjongeo ndiye angeweza kutoa vielelezo hivyo.

“Hivyo mahakama hii inaona kwamba shahidi huyo hawezi kutoa vielelezo hivyo. Kwa hiyo inakubaliana na hili pingamizi lililoletwa na mshtakiwa na inavikataa vielelezo hivi”, amesema Jaji Ndunguru.

Amehitimisha kwa kusema,  kwa kuwa sababu nyingine za pingamizi hilo zinahusiana na uwezo wa shahidi huyo kisheria, basi mahakama inaona kuwa haina sababu ya kuendelea na sababu hizo nyingine kwa kuwa sababu hii pekee inatosha kuamua pingamizi hilo.

Baada ya uamuzi huo, shahidi huyo ameomba kuwasilisha mahakamani ripoti ya uchunguzi wa uhalisia wa video hizo alizozifanyia uchunguzi.

Hata hivyo Lissu ameipinga akidai kuwa shahidi huyo hana mamlaka kwa kuwa inahusu uchunguzi wa video ambao yeye hajateuliwa kama mtaalamu.

Baada ya Lissu kumaliza kutoa hoja zake za kupinga Jamhuri imeomba ahirisho fupi ipate muda kupitia uamuzi wa video hiyo ili kuja kutoa mwelekeo utakaoisaidia mahakama kufikia uamuzi utakaokoa muda wa Mahakama.