Mahakama Kuu leo kuamua video ya Lissu

Dar es Salaam. Hatima ya picha mjongeo (video) ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu kupokelewa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili mshtakiwa huyo, kujulikana leo.

Uamuzi huo unatarajia kutolewa leo Jumatano Oktoba 22, 2025 na Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Ni uamuzi utakaomaliza ubishi ambapo upande mmoja utaibuka na ushindi baada ya mahakama kushawishika na hoja zinazodaiwa kuwa na maudhui (maneno) ya uhaini, katika mkutano wake na waliokuwa watia nia kugombea nafsi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kutishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,

Anadaiwa kuwa  Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha maneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”.

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde katika hatua ya ushahidi wa Jamhuri, ikiwa ni shahidi wa tatu.

Shahidi huyo wa tatu ni Mkaguzi wa Jeshi Polisi, Samweli Eribariki Kaaya (39), Mtaalamu wa picha, kutoka kitengo cha picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai. Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.

Katika ushahidi wake wa msingi alieleza kuwa Aprili 8, 2025 alipokea flash disk na memory card zenye video ya Lissu yenye maudhui yanayodaiwa kuwa ya uhaini,  kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Dar es Salaam kuchunguza  uhalisia wake.

Shahidi huyo, aliiomba mahakama ipokee flash na kadi hiyo ya picha mjongeo (video) ziwe kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Hata hivyo Lissu alipinga kupokewa kwa vihifadhi data hivyo vyenye video yake kuwa kielelezo akibainisha sababu nne.

Lissu alizitolea ufafanuzi wa kina katika mizania ya kisheria na msimamo wa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa mashauri mbalimbali kuhusiana na hoja hizo.

Miongoni mwa sababu hizo, Lissu alidai kuwa upokewaji wa video hizo kuwa kielelezo umekiuka kifungu cha 263(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya Mwaka 2023.

Alidai kuwa hazikuwahi kuoneshwa kwenye Mahakama ya Ukabidhi (committal court), Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kama sheria hiyo inavyoelekeza.

Sababu nyingine alidai kuwa video hizo ziliwasilishwa kabla ya wakati kwani zilipaswa zitanguliwe na taarifa ya uchunguzi wa uhalisia wake

Hata hivyo Jamhuri katika majibu yake ilipinga hoja zote za Lissu ikidai kuwa hazina mashiko ya kisheria na kuomba Mahakama izipuuze na ilitupilie mbali mapingamizi hayo.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga katika hoja ya kwanza alidai kuwa video hizo zilioneshwa katika Mahakama ya Ukabidhi huku akiialika mahakama kusoma ukurasa wa 92 na wa 93 wa kumbukumbu za mahakama ya ukabidhi.

Katuga alidai kuwa kumbukumbu za mwenendo kabidhi, zinaeleza wazi kuwa video zilichezwa kwa mshtakiwa na  matakwa ya kifungu cha 263 yametekelezwa.