Mahakama yaitahadharisha TFF kesi ya kumfungia kocha

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepinga kuendelea na usikilizaji wa kesi iliyofunguliwa dhidi yake na Kocha Liston Katabazi kwa madai kuwa wanataka kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, iliyaoamuru kesi hiyo iendelee kusikilizwa.

Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza kusilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, maarufu kama Mahakama ya Kisutu, na Hakimu Mfawidhi, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, jana Jumatatu, Oktoba 21, 2025.

Kutokana na msimamo huo wa TFF mahakama hiyo imelazimika kusimama kuendelea na usikilizwaji wa kesi na badala yake imeiahirisha hadi Novemba 13, 2023.

Hakimu Kiswaga amewataka mawakili wa TFF, Makubi Kunju na Rahimu Shabani siku hiyo kuwasilisha mahakamani taarifa ya kusudio la kukata rufaa kama ushahidi wa kuthibitisha kwamba wako katika mchakato wa kukata rufaa.

Hata hivyo, Hakimu ametoa tahadhari kuwa kama mawakili hao hawatawasilisha mahakamani taarifa ya kusudio la kukata rufaa siku hiyo, basi mahakama itaendelea na usikilizwaji wa kesi.

Katabazi anayejitambulisha kuwa mdau wa soka na kocha wa mchezo huo mwenye leseni ya daraja C iliyotolewa na TFF alifungua kesi hiyo dhidi ya Wadhamini  Waliosajiliwa wa TFF na TFF yenyewe mwaka 2024.

Alifungua kesi hiyo baada ya kufungiwa na TFF kujishughulisha na soka ndani na nje ya nchi maisha yake yote, kufuatia barua aliyoliandikia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Juni 15, 2021, akiilalamikia TFF kushindwa kusimamia soka kulingana na Sheria, Kanuni na miongozo yake.

Kutokana na barua hiyo aliitwa katika Kamati ya Maadili ya TFF, lakini  hakuhudhuria akijibu kuwa yeye si mwanachama wa TFF kwani si mwanachama wa Chama cha Makocha Tanzania (Tafca) ambacho kiko chini ya usimamizi wa TFF.

Hivyo Juni 24, 2021 TFF lilichapisha katika tovuti yake uamuzi wa kumfungia Katabazi maisha kujishughulisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi, ndipo akafungua kesi hiyo.

Katika kesi hiyo ya madai namba 14708/2024, Kocha Katabazi alidai kuwa Kamati ya Maadili ya TFF haikuwa na mamlaka ya kumpa adhabu hiyo kwani Kanuni za Maadili za TFF, Toleo la Mwaka 2021, zilizotumika kumfungia si halali.

Alidai kuwa kanuni hizo hazijasajiliwa na BMT kulingana na matakwa ya Sheria ya BMT namba 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake, hivyo kuzifanya kuwa batili kutumika kwa wanachama wake na mtu mwingine yeyote.

Pia alidai kuwa amri hiyo iliingilia haki yake ya kufanya kazi katika nyanja ya soka na hivyo kumkosesha fursa ya kupata mshahara na kipato kwa ajili ya kuendeleza maisha yake ya kila siku na familia yake, na kumsababishia maumivu ya kisaikolojia.

Hivyo aliiomba mahakama iiamuru TFF imlipe Sh600 milioni kama fidia ya madhara ya jumla aliyoyapata kutokana na uamuzi huo wa kumfungia maisha uliotolewa kwa maksudi, kimakosa na kwa nia ovu.

Pia aliomba alipwe Sh100 milioni kama fidia ya adhabu kwa kitendo cha wadaiwa kutoa uamuzi huo wakijua kuwa hawana mamlaka ya kisheria kumchukulia hatua hiyo, riba ya kiwango cha Mahakama kwa  tuzo (fedha ambazo ingeamuriwa alipwe) na gharama za kesi.

Vilevile aliiomba mahakama itoe zuio la matumizi ya Katiba na Kanuni za Maadili za TFF, akidai kuwa si vyombo halali kwa kutokusajiliwa kwa utaratibu na unaofaa.

Kocha Katabazi aliwasilisha mahakamani hapo barua ya BMT ya Juni 13, 2022 iliyothibitisha kuwa yeye si mwanachama wa TFF. Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Kiswaga, iliifuta kesi hiyo baada ya kukubaliana na pingamizi la TFF.

Hakimu Kiswaga alikubali kuwa Katabazi ni mwanachama wa TFF na kwamba kwa Katiba ya TFF, alipaswa kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya Maadili, na asingeridhika anaweza kwenda Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Hivyo alikubaliana na TFF kuwa kwa kuwa Katabazi hakufuata utaratibu huo,  mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Katabazi  alikata rufaa Mahakama Kuu  akiwakilishwa na wakili  Peter Majanjara pamoja na sababu nyingine, akidai kuwa  pingamizi la wajibu rufani halikuwa na msingi wa kisheria kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa kwenye pingamizi hilo.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Butamo  Jaji Phillip  Septemba 26, 2025, alikubalina na Rufaa hiyo, hivyo akatengua uamuzi wa Kisutu, ikaiamuru jalada lirejeshwe Kisutu iendelee kuisikiliza madai ya msingi.

Kesi hiyo ilipoitwa jana, wakili wa Katabazi, Melchisedeck Joackim ameieleza mahakama kuwa wako tayari kuendelea na usikilizwaji lakini wakili wa TFF , Kunju amesema kuwa hawako tayari kwa kuwa wanakusudia kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu

Alipoulizwa kama wana taarifa ya kusudio la kukata rufaa, ambayo ndio hatua ya awali na ya msingi ya rufaa wakili Kunju amejibu kuwa hawana kwani bado hawajaisilisha mahakamani,

Hata hivyo mesema kuwa bado wako ndani ya muda kuwasilisha mahakamani taarifa hiyo inayotakiwa kuwasilishwa ndani ya siku 30 tangu tarehe ya uamuzi, ambao unaisha Oktoba 26, 2025.

Hivyo Hakimu Kiswaga amewataka Novemba 13, 2025 kesi hiyo itakapotajwa wawasilishe mahakamani taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa kama ushahidi wa nia yao hiyo na kwamba kama hawatakuwa nayo basi kesi hiyo itaendelea kusikilizwa.