Bado nipo ughaibuni katika haya na yale kuelekea Oktoba 29 ya Watanzania kwenda kupiga kura kumchagua Rais wao na wawakilishi wao, wabunge na madiwani watakaowawakilisha bungeni na kwenye baraza la madiwani, nami pia nikiwa kwenye maandalizi ya kurejea nyumbani kupiga kura tu na kurejea ughaibuni kuendelea na mikutano.
Baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York, Marekani na Mkutano wa Uwekezaji (DICOTA) jijini Dallas, ulifuatia mkutano wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB) jijini Washington DC na sasa niko Geneva, Uswisi kwenye mkutano mkuu wa 16 wa United Nations Conference on Trade and Development (UNCTAD), ulioanza Jumatatu Oktoba 20 – 23 jijini Geneva, Uswisi.
Wakati nikihudhuria kongamano la uwekezaji DICOTA, nilipopata fursa kusalimia kongamano hilo, pia, niliwaeleza diaspora kuwa nyumbani tunajiandaa kwa uchaguzi mkuu, kama wana salaam zozote za kutuma nyumbani kuhusu uchaguzi huo, watume na mimi nitazifikisha.
Ndipo baadhi ya wana Diaspora wa Marekani wakafunguka jinsi wanavyomkubali Rais Samia Suluhu Hassan kwa makubwa anayoyafanya kwa nchi ya Tanzania na wanasema ingekuwa diaspora nao wana haki ya kupiga kura wakiwa ughaibuni kama diaspora wa nchi zingine ambao wanapiga kura kumchagua rais wao, Rais Samia angevuna kura nyingi sana za diaspora.
Hii maana yake hata maandamano ya diaspora ubalozi wa Tanzania jijini Washington DC ni kikundi tu cha watu, lakini wana diaspora wenyewe hasa wako na Samia.
Nilipowauliza sababu za kumkubali sana Rais Samia, wakasema ni kitendo cha ilani ya uchaguzi ya CCM, imeonyesha kuwa iwapo CCM ikishinda uchaguzi, itaukwamua ule mkwamo wa mchakato wa Katiba mpya, hivyo hiyo ni fursa adimu na adhimu kwa wanadiaspora kusukuma mbele upya ajenda yao ya uraia pacha.
Wanadiaspora wamesema wanamkubali Rais Samia kwa kufuatilia na kuhamasisha ushiriki wa diaspora kujenga nchi kwa kuitangaza vizuri nchi yao Tanzania ili kuvutia uwekezaji na utalii.
Huko nyuma, Rais Samia alitoa wito kwa diaspora wa Tanzania kuiweka Tanzania mioyoni mwao na kuitangaza vizuri Tanzania.
Rais Samia alisema Serikali yake inatambua na kuthamini mchango wa diaspora kwenye maendeleo ya Taifa na kuwahimiza kuendelea kuitangaza nchi kwa kusema mazuri yanayopatikana nchini ikiwemo vivutio vya utalii na fursa za biashara na uwekezaji.
Pia, Rais Samia aliwahimiza Diaspora kuendelea kuweka akiba nyumbani, kufundisha watoto wao mila na desturi nzuri za Tanzania ikiwemo lugha yetu adhimu ya Kiswahili, kupendana na kushirikiana na kufuata sheria na taratibu za nchi walizopo ili kujiepusha na changamoto zinazoweza kuwasababishia matatizo wao binafsi na nchi kwa ujumla.
Diaspora wamesema wanamkubali Rais Samia kwa kuwa amewahakikishia hali ya siasa na uchumi nchini ni nzuri na inaendelea kuimarika ambapo kwa sasa uchumi umekua kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4 miaka mitatu iliyopita na unatarajiwa kukua hadi asilimia 6.5 ifikapo mwaka 2027.
Kuhusu ajira, Rais Samia alisema bado ni tatizo, hata hivyo Serikali yake imeendelea kutafuta mbinu mbalimbali za kuwasaidia vijana na wanawake wa mijini na vijijini ili kuwawezesha kujiajiri na kujipatia kipato kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo biashara ndogondogo.
Rais Samia alisema, kwa upande wa mijini, Serikali imeendelea kuwajengea masoko bora vijana ambao wengi wanajishughulisha na biashara ndogondogo maarufu kama machinga, kuwatafutia mfuko wa kupata mitaji na kuanzisha taasisi yao ambayo inafanya vizuri na hata wameweza kuanzisha gazeti na televisheni yao.
Kuhusu vijana wa vijijini, Rais Samia alisema Serikali imeanzisha programu inayoitwa Jenga Kesho Bora (BBT) ambayo imejikita kuwawezesha vijana hao katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji.
Alisema tayari kundi la kwanza la zaidi ya vijana 800 wamepewa ekari 10 kila mmoja yenye miundombinu ya umwagiliaji na kuwakopesha mitaji na ruzuku kwa ajili ya pembejeo za kilimo.
Kuhusu sekta ya elimu na afya nchini, Rais Samia aliwaeleza Diaspora kuwa hali ni nzuri ambapo kwa sasa wanafunzi kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi kidato cha sita wanasoma bure huku Serikali ikitoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi.
Kitendo cha awamu hii ya Rais Samia kuwatambua diaspora na kuwapa hadhi maalumu, kimesababisha Rais Samia kukubalika sana na wana diaspora, hivyo hawa ndugu zetu wanadiaspora, mliopoteza uraia wa Tanzania, mnapewa hadhi maalumu, kwa kutambuliwa rasmi kupitia ‘special status’ kwa kuomba tena kurejeshewa uraia wako wa Tanzania uliopoteza, kwa kusajiliwa na kupewa kadi ya Diaspora Tanzanite Card.
Kadi hiyo itakupa haki zote za Utanzania ulizopoteza, ikiwemo kumiliki mali, hivyo Rais Samia akishinda, kwenye Katiba mpya, Tanzania na sisi tunaweza kuwa na uraia pacha.
Kwa minajili hiyo ya Rais Samia kukubalika na diaspora, kuna maana kubwa kwa umoja wetu na uzalendo wa diaspora wetu kwa nchi yetu. Mungu Ibariki Tanzania.