Dar es Salaam. Wakati zikisalia siku saba kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, vyama vya siasa vinaumiza vichwa kuhakikisha vinapata mawakala wa kutosha na waaminifu kwa ajili ya kusimamia na kulinda kura za wagombea wao.
Baadhi ya vyama hivyo, vimeeleza kutokana na uchache wa raslimali watu na fedha vitaweka mawakala maeneo machache lakini sehemu kubwa kinategemea watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Uchaguzi huo utafanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 ukishirikisha vyama 18 kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hakishiriki.
Watanzania milioni 37.6 ndiyo wenye dhamana ya kuamua nani awe diwani, mbunge na Rais kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Oktoba 29, 2025, inasuburiwa na wananchi kuamua huku vyama vya siasa vikikimbizana kuhakikisha wanakuwa na mawakala imara watakaopewa dhamana ya kusimamia kikamilifu kura zitakazopigwa siku hiyo.
Hata hivyo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), yenye dhamana ya kusimamia uchaguzi huo, imeeleza maandalizi yake yanakwenda vizuri na vifaa vyote vitakavyotumika tayari vimesambazwa kwenye Halmashauri zote Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa mujibu wa INEC, jumla ya vituo vya kupigia kura vitakavyotumika ni 99,895. Katika mgawanyo huo, Tanzania Bara itakuwa na vituo 97,348 na Zanzibar vitakuwa na 2,547.
Hii ina maana kwamba, vyama vinatakiwa kuwa na mawakala sawia na idadi ya vituo vya kupigia kura. Aidha, idadi inaweza kwenda mara tatu zaidi ikiwa chama kikiweka mawakala wa kusimamia kura za diwani, mbunge na Rais.
Mwananchi limezungumza na baadhi ya vyama vya siasa juu ya maadalizi hususan eneo la mawakala ambapo kila chama kina mpango wake kuwapata wawakilishi hao kwenye vituo vya kupigia kura. Ukata ukitajwa kuwa kikwazo.
Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), John Mrema, amesema chama hicho kinahitaji zaidi ya watu 100,000 watakaotumika kama mawakala wa wagombea wao kuanzia ngazi ya kata, majimbo hadi urais.
“Shughuli hiyo inaendelea ili kuhakikisha tunapata mawakala waaminifu watakaosimamia na kulinda kura za wagombea wetu,” amesema Mrema.
Chama cha ACT-Wazalendo, Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, amesema maandalizi ya ndani yanaendelea kwa kasi kubwa, ambapo timu za wagombea zinafanya juhudi kuhakikisha kila kituo cha kupigia kura kinakuwa na wakala.
“Tumejipanga kushiriki uchaguzi huu kwa lengo la kushinda majimbo na kata nyingi iwezekanavyo. Tunahakikisha tunakuwa na mawakala kila eneo ili kulinda kura zetu,” amesema Semu.
Semu amesema bado kuna changamoto za kiutendaji kutoka kwa baadhi ya wasimamizi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), hasa kuhusu ucheleweshaji wa utoaji wa barua za kiapo kwa mawakala.
“Tumeendelea kupokea taarifa kutoka maeneo mbalimbali kuwa baadhi ya mawakala wetu hawajapokea barua za kiapo, jambo linalotofautiana kulingana na majimbo na kata,” amesema.
Amesema umuhimu wa kuwa na mawakala wenye uwezo na uaminifu, akieleza wao ndio walinzi wa kura na kwamba vyama vya upinzani vimekuwa vikikumbana na changamoto za muda mrefu kuhusu uapishaji wa mawakala kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa amesema chama hicho kinatekeleza kwa umakini mkubwa shughuli ya kupata na kuwasimamia mawakala kama ilivyoelekezwa na sheria za uchaguzi.
“Sehemu zote tulizosimamisha wagombea, mawakala wamejitokeza. Tunatarajia ifikapo Oktoba 22, 2025 wote watakuwa wameapishwa,” amesema Ngulangwa.
Kwa upande wake, Moshi Kigundula, Katibu Mkuu wa UMD amesema chama chao kiko katika hatua za mwisho za kuandaa barua kwa mawakala wao ili wawasilishe kwa INEC na kuapishwa rasmi.
“Tunaamini tutakamilisha hatua hii, na kila sehemu tuliyoweka mgombea tutakuwa na wakala wake,” amesema Kigundula.
Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo amesema chama hicho tayari kimeshaandaa barua za kuwatambulisha mawakala wao na kwa sasa wanazigawa kwao ili kutoa nafasi ya kwenda kuapishwa na INEC.
“Tumejipanga si utani na wote wanapewa barua za utambulisho ili wakaapishwe na kusubiri siku ya Uchaguzi,” amesema.
Kaimu Mwenyekiti wa DP, Abdul Mluya amesema wanaendelea kujipanga na mawakala na kuwaapisha akiwasisitiza wanachama wa chama hicho kutoa michango yao kusaidia malipo ya mawakala.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Bertha Mpata amesema wanajiandaa mawakala wakaapishwe.
Hali ni tofauti kwa Chama cha UPDP ambapo Mwenyekiti wake, Twalib Kadege amesema hawana fedha za kuweka mawakala.
“Tunaukata wa fedha za kuweka mawakala nchi nzima, kampeni zenyewe tumefanya kwa shida hivyo hatutaweka mawakala kutokana na fedha za kuwalipa,” amesema
Pia, Mwenyekiti wa NRA, Khamis Faki amesema wameweka mawakala baadhi ya maeneo na mengine ambao hawataweka mawakala watawatumia wale wa INEC.
“Changamoto ni fedha, tutaweka mawakala baadhi ya maeneo na maeneo mengine tutawatumia wale wa INEC,” amesema.
Katibu Mkuu wa Chama cha AAFP, Rashid Rai amesema hawana fedha za kuweka mawakala kila mkoa.
“Hatuna cha kuwalipa mawakala, tutachukua baadhi ya maeneo ambayo tumesimamisha wagombea maeneo mengine tutaomba wajitolee na maeneo tutaomba Mungu atusaidie,” amesema.
Jitihada za kukipata Chama cha Mapinduzi (CCM), kujua maandalizi yake kwa mawakala hazikuzaa matunda kwani hakuna kiongozi aliyepatikana.
Hata hivyo, Mwananchi linajua kwamba maandalizi yanaendelea kwa mawakala wao watakaokuwapo kwenye kila kituo cha kupigia kura nchi nzima.
Kifungu cha 77 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya Mwaka 2024 ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kinasema kila chama cha siasa kinaweza, baada ya kupata ridhaa ya wagombea, kuteua mtu mmoja atakayejulikana kama wakala wa upigaji kura kwa kila kituo ndani ya jimbo au kata ambayo ina mgombea au wagombea kwa madhumuni:-
(a) kuwabaini watu wanaodanganya kuwa wanastahili kupiga kura; (b) kumwakilisha na kulinda maslahi ya mgombea au wagombea katika kituo cha kupigia kura na (c) kushirikiana na msimamizi wa kituo na wasimamizi wasaidizi wa kituo ili kuhakikisha sheria na taratibu zinazohusu upigaji kura na chaguzi zinazingatiwa katika kituo.
Majukumu makuu ya wakala ni pamoja na wakati wa upigaji kura kutambua na kuthibitisha wapiga kura: kuhakikisha kila mpiga kura anayepiga kura ni mkazi halali wa eneo hilo, yupo kwenye Daftari la Wapiga Kura, na ana sifa za kisheria kupiga kura katika kituo hicho.
Kufuatilia kwa karibu utaratibu mzima wa upigaji kura ili kuhakikisha hakuna makosa, udanganyifu, au uvunjifu wa sheria unafanyika (mfano: kupiga kura mara mbili).
Pia, kutunza amani na utulivu kusaidia maofisa wa uchaguzi kutunza utulivu katika kituo cha kupigia kura. Wakati wa kuhesabu kura na matokeo kuangalia kuhesabu kura: kuhakikisha hesabu ya kura inafanyika kwa uwazi na kwa kufuata utaratibu na kwamba kura zilizoharibika zinatengwa kwa usahihi.
Kupokea Nakala ya Matokeo: Ni jukumu lake la kisheria kupokea nakala halisi ya fomu ya matokeo ya kura (mfano Fomu Na. 11/12/14) ambayo imejazwa na kusainiwa na msimamizi wa kituo, kabla haijapelekwa kwenye kituo cha kujumlishia. Hii ndiyo sehemu muhimu zaidi ya kazi yake.
Wakati hayo yakielezwa hivyo, INEC imesema maandalizi yapo katika hatua nzuri, wasimamizi na wasaidizi wa vituo wapo na usahili umeanza maeneo mbalimbali na utaratibu wa utoaji wa mafunzo unaendelea.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima akizungumza na Kituo cha Habari za Chanel ten, amesema usambazaji wa vifaa tayari umefanyika katka halmashauri zote Tanzania bara na Zanzibar na kampeni za uchaguzi zinaendelea.
Amepongeza vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi wa mwaka huu akieleza hakuna mgongano wala mivutano baina ya chama na chama kwenye kampeni wala hawajapokea malalamiko yeyote kupitia kamati za maadili kwa wagombea wa nafasi ya urais.
“Hata kwenye majimbo malalamiko yanayokuja ni machache ngazi ya maadili, mfano Kigoma kulitoka mvutano baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo na yalishughulikiwa,” amesema.
“Tathmini yetu sisi tunakwenda vizuri, na tunaamini watu watajitokeza kupiga kura kutokana na wingi wao wanavyojitokeza kwenye mikutano ya kampeni nafasi ya urais kusikiliza wagombea wakinadi sera zao,” amesema.
Kulingana na maelezo ya Kailima amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 162 ya sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya 2024 iliweka utaratibu, chama chochote cha siasa kinachopenda kushiriki uchaguzi sharti lazima kishiriki mchakato wa kupata kanuni za maadili ya uchaguzi.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameeleza kutokuwa na elimu ya kutosha ya uraia kuhusu uchaguzi huo kwa kile wanachodai Serikali imekuwa mstari wa mbele zaidi kuliko wapigakura kuwahamasisha zaidi kwenda kupiga kura bila kuwaeleza manufaa ya kufanya hivyo.
Kauli ya baadhi ya wananchi, wanadai, bado kuna sintofahamu kuhusu utaratibu wa kupiga kura, utambuzi wa wagombea na wajibu wao kushiriki uchaguzi kwa uelewa mpana.
“Sijaju bado nitapigia wapi kura na sina uhakika wagombea wetu ni akina nani hasa maana sina taarifa za kutosha, wagomea wengi kwa sasa sio maarufu na sio wale ambao tumezoea kuwaona kwenye majukwaa ya kisiasa,” Said Mushi, mkazi wa Temeke Dar es Salaam.
Mwananchi mwingine, Emmanuel Kasembo (63), Mkazi wa Kelege, Amani willayani Bagamoyo mkoani Pwani, amesema kampeni za uchaguzi wa mwaka huu zimepoa tofauti na chaguzi zilizopita hali inayoshusha morari ya watu kujitokeza kupiga kura. “Pia hizi habari za maandamano siku ya uchaguzi zimeenea zinatia hofu, wengi wanasema siku ya uchaguzi itakuwa siku ya mapumziko ya kukaa ndani ili kuepuka vurugu zinazoweza kutokea,” amesema.
Kasembo amesema elimu bado haijawafikia kikamilifu kwani baadhi ya vyama tu ndio wanafanya mikutano ya hadhara ingawa hawafafanui vizuri thamani ya kura.
Mtazamo huo wa wananchi hauna tofauti na alioutoa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (udom), Conrad Masabo akisema hali ya kampeni za mwaka huu imekuwa tofauti na miaka mingine akitaja kuwa inaibua maswali kadhaa kampeni zikielekea mwisho. “Kampeni za miaka ya nyuma hazikuwa zinapambwa na wananchi waliovaa sare aina moja, kampeni za mwaka huu ukiangalia kila chama unaona wananchi waliovaa sare za chama hicho pekee.
Swali la msingi hapa linaibuka kuwa wanaohudhuria mikutano ni wanachama pekee na kama ni hivyo, je hawa wananchi wengine hawashiriki kampeni hizo,” amehoji.
Dk Masabo amedokeza kampeni za mwaka huu kumekuwa na madai ya matumizi ya rushwa maeneo mbalimbali ambapo video tofauti zimekuwa zikisambazwa kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii na kuathiri taswira ya uchaguzi wenyewe.
Amesema zamani kampeni za kisiasa kila mgombea alikusanya wananchi na makundi mbalimbali kusikiliza sera zake tofauti na mwaka huu huenda ikaashiria kushuka molari ya wananchi kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi.