Mgombea ubunge wa Chaumma abadili gia, azisaka kura mtaa kwa mtaa

Mbeya. Zikiwa zimebakia siku saba Watanzania wapige kura katika Uchaguzi Mkuu wa Jumatano  Oktoba 29, mgombea ubunge wa Jimbo la Uyole  kupitia Chama cha Ukombozi  wa Umma (Chaumma), Ipyana Njiku ameanza kuzisaka kura mtaa kwa mtaa.

Miongoni mwa maeneo ambayo anayafikia kwa urahisi ni pamoja na vijiwe vya bodaboda, bajaji wakiwepo kina mama wajasiriamali wa mboga na matunda  kwenye masoko.

Staili ya mgombea huyo imekuwa kivutio na kukusanya  wananchi wakiwepo kina mama kusikiliza sera  zake na nini atatekeleza  endapo  akipewa ridhaa ya kuwatumikia.

Awali, akizungumza  na wananchi  wa makundi  mbalimbali, Njiku ametaja  moja ya kipaumbele  cha kwanza ni kutatua  hadha ya maji katika Bonde  la Uyole sambamba na ujenzi wa soko la kisasa ili kuondoa  hadha  kina mama kukaa juani.

Njiku amesema  yeye ni mkazi  Kata ya Nsalaga Bonde la Uyole, anatambua  kero ya maji iliyopo kwa kipindi  kirefu, endapo akipata ridhaa  atahakikisha  anaishawishi Serikali kufikisha huduma  ya maji safi na salama  kutoka  chanzo cha  Ziwa Nyasa Wilaya ya Kyela.

“Nimekuja kuomba kura zenu Oktoba 29, mwaka huu mkachague Chaumma, kwani natambua kuna tatizo kubwa la maji safi na salama na nyinyine nyingi,  ndio sababu iliyo nisukuma kuja kwenu  kuomba ridhaa ya nafasi hii niwe mwakilishi wenu bungeni mjini Dodoma,” amesema.

Mgombea  ubunge  Uyole kupitia Chama cha Ukombozi  wa Umma(Chaumma),Ipyana Njiku akizungumza  na mmoja wa  wajasiriamali  Soko la Uyole wakati  akiomba kura na kuhamasisha kujitokeza kushiriki uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025. Picha na Hawa Mathias

Njiku, amesema mbali na kuboresha huduma ya maji, lakini watazingatia  vipaumbele  vya wananchi  lengo  ni kuona wanafikishiwa huduma  karibu zikiwepo  sekta ya elimu na afya.

“Tunajua changamoto  za wananchi  nimekuja kwenu mtupe kura za kishindo za nafasi ya Rais, wabunge  na madiwani kwenye  uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025, ili tuweze kufanya yale tulio waeleleza kwenye mikutano ya kampeni lengo ni  kuleta maendeleo  kwa wana Uyole,”amesema.

Mkazi wa Uyole, David  Aloyce amesema  wao wako kuangalia sera na chama kitakacho leta maendeleo  kikubwa ni  kuibua changamoto  za wananchi na kuzitatua hususani  katika  kusimamia sera zao.

“Wagombea mbalimbali wanakuja na sera zao za kuleta maendeleo  wa Watanzania, lakini wanapaswa kutambua  kura ni siri ya mpiga kura ambaye anajua nani atampigia,” amesema.