Mgombea urais TLP aahidi kuinua uchumi kupitia kilimo, ufugaji

Vunjo. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira, ameahidi endapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi, ataimarisha uchumi wa Taifa kwa kuwekeza zaidi katika sekta za kilimo, ufugaji na utalii.

Rwamugira ametoa ahadi hiyo leo wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Mwika Sokoni, jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro, ambapo amewasihi wananchi kumpa ridhaa ya kuunda serikali itakayojali maendeleo ya Watanzania wote.

“Katika Ilani ya TLP tunasema tunataka utawala bora, wa haki na wa kisheria. Tutaulinda na kuuheshimu Katiba ya nchi yetu, huku tukihakikisha kila Mtanzania ananufaika na rasilimali za taifa,” amesema Rwamugira.

Amesema serikali yake itaimarisha uchumi wa wananchi kwa kusimamia vizuri rasilimali zilizopo nchini, ikiwemo ardhi yenye rutuba, madini, milima, mito na mbuga za wanyama.

“Tuna kila kitu rasilimali watu, ardhi, mito, milima na wanyama. Kila mmoja akifanya kazi tutaimarisha uchumi wetu. Tukiuza ndizi, nyama na bidhaa za utalii, taifa litakuwa na kipato cha kutosha,” ameongeza.
 

Miundombinu na huduma za kijamii

Rwamugira ameahidi kuboresha miundombinu ya barabara nchini ili kurahisisha usafiri wa watu na mizigo, na kuwezesha watalii kufika kwa urahisi kwenye vivutio mbalimbali.

“TLP tutashughulikia barabara zote zisizopitika hasa vijijini. Kwani ili watalii wasafiri na kuleta fedha, watu wa madini na hata wakulima kusafirisha mazao, lazima tuwe na barabara nzuri,” amesema.

Akizungumzia huduma za jamii, mgombea huyo ameahidi matibabu bure kwa Watanzania wote endapo TLP itaunda serikali, na kwamba kila kata itakuwa na kituo cha afya au hospitali yenye vifaa tiba na wataalamu wa kutosha.

“Mgonjwa akifariki hospitalini, ndugu hawatatozwa fedha. Watakabidhiwa mwili bila gharama ili kwenda kuzika,” amesema.

Kuhusu elimu, Rwamugira ameahidi elimu bure kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu, bila michango yoyote ya jengo au ulinzi, akisema serikali yake itagharamia gharama zote za elimu.

Amesisitiza pia kuwa mikopo ya elimu ya juu itafutwa na badala yake serikali itahakikisha wanafunzi wote wanasoma bure huku wakijifunza ujuzi wa ufundi utakaowawezesha kujiajiri.

Katika kukabiliana na changamoto ya ajira, Rwamugira amesema serikali yake itaweka mfuko wa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo, mama lishe, waendesha bodaboda na bajaji, ambapo watapewa mikopo yenye masharti nafuu na kulipa kidogo kidogo.

Amesema pia serikali itajenga viwanda vidogovidogo katika kila eneo ili kuongeza thamani ya mazao, kuendeleza sekta ya mifugo na kuwezesha wananchi kupata kipato.

“Wafugaji vijijini watajengewa majosho, vijana watafundishwa ufundi na wazee watapatiwa msaada maalum. Tunataka kila mmoja awajibike na afanye kazi,” amesema.
 

Wito wa amani na ushiriki wa uchaguzi

Rwamugira amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura kwa amani na utulivu, huku akisisitiza kuwa uchaguzi ni haki ya kikatiba na ni utaratibu unaofanyika kila baada ya miaka mitano.

“Siku ya uchaguzi ondoka asubuhi, nenda kituoni, piga kura yako, kisha rudi nyumbani uendelee na shughuli zako. Usitishike na uwepo wa polisi au wanajeshi kama utawaona barabarani, wale wako kwa ajili ya kuhakikisha usalama wetu,” amesema.

Ameongeza kuwa wale wanaodai uchaguzi hautafanyika ni waongo, kwani Katiba ya Tanzania inaweka wazi utaratibu wa uchaguzi wa kidemokrasia.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Vunjo kupitia TLP, Richard Lyimo, amewaomba wananchi wamchague ili awe sauti yao ndani ya Bunge, akiahidi kupambana na changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

“Siendi kujifunza ubunge, nakwenda kufanya kazi ya ubunge. Nitumeni nifanye kazi, nina uchungu na wananchi wa Vunjo,” amesema Lyimo.

Lyimo ambaye ni mwenyekiti wa TLP Taifa, ametumia pi nafasi hiyo kuonya wananchi kuepuka rushwa wakati wa uchaguzi, akisema rushwa hupofusha macho na kuzuia maendeleo.

Amesema akipewa nafasi ya ubunge, ataondoa mfumo wa mikopo kandamizi unaoitwa kausha damu, na badala yake atawezesha vijana kupitia viwanda vidogo na mafunzo ya ufundi ili waweze kujiajiri.

“Kina mama na vijana, mkinichagua hakutakuwa tena na kausha damu, tutaanzisha viwanda na miradi ya vijana. Nitakuwa mbwa wenu wa kubweka bungeni kuhakikisha nawatetea wananchi ili kupata maendeleo ya kweli,” amesema Lyimo.