Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, John Heche, amekamatwa leo asubuhi akiwa anaingia katika viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Heche amekamatwa leo Jumatano, Oktoba 22, 2025 nje ya Mahakama hiyo, wakati akijiandaa kwenda kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Pia, leo kesi ya kudharau amri ya Mahakama inayowakabili viongozi wa Chadema akiwemo Katibu Mkuu wa Chama hicho, John Mnyika pamoja na Heche imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Awamu Mbagwa.
Akizungumza leo Oktoba 22, 2025 na waandishi wa habari katika viunga vya Mahakama Kuu, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amedai kuwa Heche alikamatwa ghafla na askari polisi wakati akiingia katika lango la mahakama hiyo, na baada ya kukamatwa amepelekwa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.
Mnyika amesema kuwa hadi sasa chama hakijapewa taarifa rasmi kuhusu sababu za kukamatwa kwa Heche, huku akieleza timu ya mawakili wa chama hicho imeelekea kituoni kufuatilia tukio hilo.
“Tumepokea taarifa kwamba Makamu Mwenyekiti wetu, John Heche, amekamatwa muda mfupi kabla ya kuingia mahakamani. Amepelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, lakini hatujajulishwa sababu rasmi za kukamatwa kwake,” amesema Mnyika wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Mnyika amedai kuwa tukio hilo ni mwendelezo wa kile alichokiita ‘njama dhidi ya viongozi wa Chadema’, akieleza kuwa hata yeye pamoja na baadhi ya viongozi wengine waandamizi wa chama hicho wana wasiwasi kwamba huenda wakakamatwa muda wowote.
“Hili si jambo jipya. Tumekuwa tukipata taarifa za uwepo wa mpango wa kuwakamata viongozi wetu tangu muda mrefu. Hata mimi niko huru kwa sasa, lakini sina uhakika kama sitakamatwa muda wowote,” ameongeza.
Mpaka sasa bado Jeshi la Polisi halijatoa taarifa rasmi ya kumshikilia kiongozi huyo.
Endelea kufuatilia mitandao ya kijamii ya Mwananchi