STAA wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Alphonce Modest anatarajiwa kuzikwa Ijumaa, Agosti 24, 2025 mchana katika makaburi ya Lubengela mkoani Kigoma.
Kwa mujibu wa mdogo wake, Agustino Modest aliyekuwa anamuuguza kwa kipindi chote hicho ametoa ratiba itakavyokuwa akisema ratiba itaanza siku hiyo asubuhi.
“Ijumaa asubuhi tutaaga mwili hapa nyumbani mtaa wa Kisangani, Mwanga Kaskazini (Kigoma), kisha tutakwenda kanisani kwa ajili ya misa takatifu itakayofanyika Kanisa la Roman Katoliki la Bikira Maria Mshindani. Baada ya hapo tutakwenda kumpumzisha,” amesema Agustino.
“Kwa sasa tunaendelea kupokea wageni mbalimbali wanaokuja kutuona na kuwasubiri watoto wake ambao ni Kelvin yupo Morogoro, Rachel yupo Mwanza na Vicky yupo Arusha.”
MANENO YA MWISHO YA ALPHONCE
Agustino amesema kabla ya kaka yake kufariki dunia alimwambia kwamba ahakikishe wanawe wanawajua ndugu.
“Hakikisha wanangu wanawajua ndugu zao na waje kunizika. Pia naomba umwambie Nteze John kwamba sipo tena duniani, pia alinishukuru kwa kumuuguza kwa kipindi chote na kuacha kila kitu. Baada ya muda hali yake ikabadilika na akaaga dunia,” amesema Agustino.
Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na baba mzazi wa mchezaji huyo, mzee Modest Songoro aliyesema.”Bado nina maumivu makali mno. Siyo kazi rahisi baba kumzika kijana wake, Alphonce ni kijana wangu wa kwanza.”
“Nimeshuhudia maumivu makali ya kijana wangu toka anaugua hadi anaondoka duniani kwa takriban miaka 15. Moyo wangu umevunjika. Acha kwanza tuzike huenda nitakuwa nimetulia.”