Mtasingwa: Azam FC tunaandika historia

LICHA ya kuwa nje ya uwanja akiuguza majeraha, kiungo wa Azam FC, Adolf Mtasingwa amesema kesho Ijumaa historia itaandikwa kwa klabu hiyo kutinga hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza huku akiwapongeza nyota wa timu hiyo kwa kuipambania nembo ya klabu.

Mara ya mwisho kuonekana uwanjani kwa kiungo huyo mkabaji ilikuwa ni Februari 15, 2025 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa ambapo Azam FC iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mtasingwa alisema anaiona nafasi kubwa ya Azam kutinga hatua ya makundi ikiwa na mtaji wa mabao mawili ya ugenini ilionao dhidi ya KMKM huku akiweka wazi kuwa ni wakati sahihi kufanya kila linalowezekana ili kuiheshimisha timu hiyo.

“Nafurahishwa na kinachofanywa na wenzangu wanapambana na naona wakifikia malengo ya kutinga hatua ya makundi kama mipango ilivyokuwa baada ya kupata nafasi ya uwakilishi kimataifa, mtaji wa mabao mawili ya ugenini umepunguza presha.

“Ijumaa kazi ni moja tu, kufanya vizuri kwa kutumia kila nafasi itakayotengenezwa, nina imani kubwa na benchi la ufundi sambamba na wachezaji ambao wameonyesha kuwa na uhitaji mkubwa kuandika historia kwa kutinga hatua ya makundi kwa mara ya kwanza,” alisema.

Akizungumzia afya yake kwa ujumla, kiungo huyo alisema anaendelea vizuri na anaamini muda sahihi utaamua yeye kurudi kuendelea kuipambania timu.

“Juu ya kurudi uwanjani hapo tumuachie Mungu atende kwa vile anavyotaka kwa maana ndio namna pekee inawezekana, natambua wengi wananiombea nirejee uwanjani haraka iwezekanavyo, mimi pia natamani iwe hivyo, muda ukifika nitarudi na nitafanya kazi yangu,” alisema.

Pamoja na kukosekana kwake akiwa panga pangua kikosi cha kwanza kabla ya ujio wa Florent Ibenge, kiungo huyo atakuwa na kibarua atakaporejea kutokana na mabadiliko ya benchi la ufundi lakini pia ongezeko la nyota wanaocheza nafasi moja.

Azam FC imeongeza nyota eneo la kiungo mkabaji ambao ni Himid Mao, Sadio Kanoute wote wakiwa ni wachezaji wapya.