Profesa Assad: Hali ya kiuchumi Tanzania ni nzuri

Morogoro: Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM), Profesa Mussa Assad amesema hali ya kiuchumi nchini Tanzania ni nzuri na inaendelea kuimarika kwa kasi, jambo linaloashiria mafanikio makubwa ya Serikali ya awamu ya sita katika kusimamia uchumi jumuishi unaogusa wananchi wa kada zote.

Profesa Assad, amebainisha hayo katika kongamano la kitaaluma la kujadili utekelezaji wa uchumi jumuishi kuelekea Dira ya Taifa ya 2050, akisema uchumi ni jambo linaloweza kutathminiwa na kila Mtanzania kwa mujibu wa maisha yake ya kila siku.

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya sasa uchumi umekuwa kwa wastani wa karibu asilimia 6, huku mfumuko wa bei ukiendelea kudhibitiwa vizuri.

Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi, David Kafulila.

“Kwa vigezo vya kiuchumi, Tanzania ipo katika nafasi nzuri sana, mfumuko wa bei uko chini wananchi wana uwezo wa kupata chakula na kuhudumia familia zao ukilinganisha na nchi jirani kama Kenya na Rwanda, sisi tumekaa vizuri,” amesema Assad, ambaye pia aliwahi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi, David Kafulila, amesema mafanikio ya uchumi wa Tanzania yanatokana na uamuzi mzuri wa Serikali kuwekeza kwa kiasi kubwa katika sekta ya kilimo, hasa katika miundombinu ya umwagiliaji umechangia kuongeza uzalishaji na kipato cha wananchi vijijini.

“Miaka minne iliyopita tulikuwa na hekta 540, 000 za umwagiliaji, lakini sasa tumefikia karibu 1,000,000, huu ni uamuzi wa kimkakati unaoongeza tija katika kilimo na kusaidia kupunguza umasikini,” amesema Kafulila.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Moshi James amesema ili kufanikisha Dira ya Taifa ya 2050 kuna haja ya kuongeza uwajibikaji katika sekta ya umma na kuimarisha ubia na sekta binafsi.

“Bajeti ya Serikali pekee haiwezi kutatua changamoto zote za maendeleo, tukitumia vizuri rasilimali binafsi na ubia tutaongeza kasi ya maendeleo,” amesema Dk Moshi.

Kongamano hilo linalenga kuhamasisha wadau kuendelea kushirikiana katika kujenga uchumi imara, jumuishi na endelevu kuelekea mwaka 2050.