Dar es Salaam. Wakati wengi wakiamini kuwa saratani ya matiti ni ugonjwa wa wanawake pekee, kwa Ramadhani Rashid Mussa (57), mkazi wa Mbezi Malamba Mawili, imani hiyo ilivunjika mwaka 2023 baada ya madaktari kubaini kuwa uvimbe uliokuwa ukimtesa kifuani kwake kwa muda mrefu ulikuwa saratani ya titi.
Safari yake ya maumivu, sintofahamu, na matumaini ilianza mwaka 2005, alipogundua titi lake likitoa majimaji meupe.
“Nilianza kuona sehemu ya titi langu linatoa maji meupe,” anaanza simulizi yake kwa sauti tulivu lakini yenye kumbukumbu nzito. “Nilipokwenda hospitali, walisema ni hali ya kawaida ya homoni. Nilipuuza nikaendelea na maisha.”
Miaka ikasonga, lakini kadri siku zinavyoenda, alishtuka ghafla fulana yake inaloa na shati halikadhalika limeshachafuka. “Unashangaa watu wanakushangaa nguo imeshachafuka.”
Alifikiri tatizo limeisha hapo, lakini mwaka 2020, alianza tena kuhisi maumivu makali kifuani. “Nikaanza kuona kuna vichomi vinachomachoma kwenye titi. Nilirudi hospitali, wakasema labda itakuwa ni ziwa tu linakua. Nikapuuza,” anasema huku akitikisa kichwa, kana kwamba bado haamini alivyochukulia jambo kwa urahisi wakati huo.
Ugonjwa unaojificha kimya kimya
Ramadhani anasema alianza kujisikia vibaya zaidi mwaka 2023 akiwa kazini mkoani Mtwara. “Nilianza kupata maumivu makali sana. Niliporudi Dar es Salaam, nikakwenda hospitali ya Mwananyamala, vipimo vya awali vilionesha hakuna tatizo, lakini nilihisi tofauti nilijua mambo hayako sawa.”
Alipelekwa kwa rufaa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na baada ya vipimo vya kina zaidi, madaktari walithibitisha kuwa alikuwa na saratani ya matiti hatua ya pili, na tayari uvimbe ulikuwa umeanza kusambaa.
“Sikuwahi kufikiria mwanaume anaweza kuugua saratani ya matiti. Nilishangaa na nikahisi dunia imenigeuka,” anasema kwa huzuni.
Ramadhani alipatiwa rufaa kwenda Taasisi ya Saratani Ocean Road, ambako alianza matibabu ya dawa za kemikali (chemotherapy). “Nilianza na dozi nne za mwanzo, kila baada ya siku 21. Kila dozi ilikuwa mateso kutapika, kuharisha, mwili kuishiwa nguvu. Ukirudi nyumbani, unalala siku 10 hadi 12, hujisikii kufanya chochote,” anasema.
Baada ya miezi mitatu, madaktari walimfanyia upasuaji kuondoa uvimbe mkubwa kifuani. “Walipofungua, walikuta umeenea zaidi ya walivyotarajia. Baada ya upasuaji walitumia asali na dawa mbalimbali kusaidia kidonda kupona kabla ya kunifanyia ‘skin graft’, walitoa kipande cha nyama ya paja na kubandika kifuani. Nilikuwa na vidonda viwili kwa wakati mmoja,” anasema huku akikumbuka maumivu hayo.
“Nilijifunza kuwa tiba ya saratani si mchezo. Wale wanaoitwa mashujaa wa saratani kweli ni mashujaa, kwani ni mateso, lakini pia ni matumaini,” anasema kwa msisitizo.
Baada ya kupona jeraha, aliendelea na kemotherapi nyingine nne, kisha akaanza mionzi tiba (radiotherapy). “Kila siku isipokuwa Jumamosi na Jumapili nilikuwa napigwa mionzi kwa siku 25. Ukiwa pale, hujui kinachotokea, unaona tu mashine inazunguka, lakini ndani mionzi inaua seli za saratani.”
Leo hii, Ramadhani anasema afya yake imerejea. “Nilirudi kliniki, daktari akaniambia niko sawa. Kwa sasa nahudhuria kila miezi mitatu. Nilipoteza uzito hadi kilo 49, uliporudi na kufikia 55. Niliona nuru tena na baadaye uzito wangu wa kawaida ukarejea,” anasema kwa tabasamu dogo.
Siri aliyoibeba mwaka mzima
Ramadhani hakumwambia mkewe kuhusu ugonjwa huo kwa zaidi ya mwaka mmoja. “Niliona nikimwambia mapema atapata presha. Ijapokuwa nyakati zote alijua kuwa naumwa, sikumweleza nasumbuliwa na nini. Nilimwambia baada ya kufika Ocean Road,” anasema.
Anasema majibu hayo yalisababisha mshtuko mkubwa nyumbani. “Mke wangu alinikasirikia sana, akaniambia, ‘Mbona hukuniambia mapema?’ Nyumba ilivurugika kidogo, lakini baada ya muda tulikubaliana kwamba si vizuri kuficha tena mambo kama haya.”
Hadi sasa, mama yake mzazi hajui mtoto wake alipitia ugonjwa huo. “Anaishi na mdogo wangu, na sikutaka ajue. Nilihofia kumuumiza kihisia, kwani naye anaugua presha,” anasema.
Kwa mujibu wa madaktari wa Ocean Road Cancer Institute, takribani asilimia tano ya wagonjwa wote wa saratani ya matiti nchini ni wanaume.
“Wanaume wengi huona aibu au hudhani ni kitu kidogo kama kuvimba kwa homoni. Wanakuja hospitalini ugonjwa ukiwa umechelewa. Ndiyo maana elimu ni muhimu,” anasema.
Dalili zake kwa wanaume ni pamoja na titi kutoa majimaji, uvimbe kifuani, maumivu au ngozi kubadilika, lakini wengi huzipuuzia.
Ramadhani anakiri alichelewa kwa sababu hiyo hiyo. “Kama ningeenda mapema, labda nisingefanyiwa upasuaji mkubwa, lakini Mungu aliniokoa,” anasema.
Gharama kubwa, uelewa mdogo
Licha ya huduma nzuri anazozipongeza Ocean Road, anasema gharama za matibabu bado ni changamoto kubwa. “Mtu mpaka aitwe shujaa ni kweli, maana unapitia mateso makubwa ya kimwili na kifedha. Binafsi nilitumia zaidi ya Sh6 milioni. Gharama ni kubwa, na si kila familia inaweza kumudu,” anasema.
Anatoa wito kwa Serikali kuweka utaratibu maalumu wa kupunguza gharama za matibabu ya saratani kwa wananchi wenye kipato cha chini. “Wapo watu wanakufa majumbani kwa sababu ya gharama. Familia inasema, ‘si bora abakie nyumbani?’ Hii ni hatari.”
Hata hivyo, anakiri kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika upatikanaji wa dawa na vifaa, lakini bado uhitaji ni mkubwa. “Tumepanua huduma hadi mikoani, lakini elimu ya mapema ndiyo itasaidia zaidi kupunguza gharama na vifo,” anasema.
Sasa, Ramadhani anajitambulisha kama mshindi wa saratani ya matiti. “Niliona watu waliopona Ocean Road, na hilo lilinipa nguvu. Nilijiambia, kama wao wamepona, hata mimi nitapona,” anasema.
Anapaza sauti yake kwa wanaume wenzake: “Wababa, saratani ya matiti ipo. Ukiona titi lako linatoa majimaji yasiyo ya kawaida au unahisi uvimbe, haraka nenda hospitali. Usichelewe. Ugonjwa ukigundulika mapema unatibika.”
Anasisitiza kuwa hakuna ugonjwa wenye aibu. “Wengine wanaona ni aibu mwanaume kuwa na saratani ya matiti. Sio aibu; ni ugonjwa kama mwingine. Muhimu ni kutafuta tiba mapema,” anasema kwa ujasiri.
Kwa sasa, Ramadhani anaendelea na tiba ya ufuatiliaji (follow-up therapy) kila miezi mitatu na anatarajiwa kumaliza raundi ya kwanza ya dawa zake za miezi sita Novemba mwaka huu.
“Maisha yamebadilika, lakini nimejifunza thamani ya afya. Afya ni kila kitu,” anasema.