Simba yaingia 10 bora tuzo za CAF 2025, Pyramids, Berkane ndani

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeiweka Simba katika orodha ya timu 10 zinazowania tuzo ya Klabu Bora ya soka mwaka 2025 kwa wanaume.

Mafanikio ambayo Simba imeyapata mwaka huu kwa kuingia Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024/2025 yameonekana kuibeba na kuifanya iingie katika kundi hilo la Klabu 10.

Orodha hiyo inajumuisha idadi kubwa ya timu ambazo zilifanya vizuri katika mashindano ya Klabu Afrika msimu uliomalizika.

Mabingwa wa Taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/2025, Pyramids FC wapo kundi na wanaonekana kuwa katika nafasi kubwa ya kuibuka washindi kwa vile hivi karibuni waliongeza Taji la CAF Super Cup.

Orodha haijawaacha mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, RS Berkane ambao wiki iliyopita wamechapwa bao 1-0 na Pyramids FC katika Fainali ya CAF Super Cup.

Klabu za Afrika Kusini zimetawala katika orodha hiyo kwa vile ziko tatu, zikifuatiwa na zile za Algeria ambazo zimeteuliwa mbili na nyingine zilizobakia ni kutoka nchi za Morocco, Misri, Tanzania, Sudan na Ivory Coast.

Timu hizo zinazowania tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka 2025 Afrika ni CR Belouizdad na CS Constantine (Algeria), Orlando Pirates, Mamelodi Sundowns na Stellenbosch (Afrika Kusini), Pyramids FC (Misri), Asec Mimosas (Ivory Coast), Simba (Tanzania), Al Hilal (Sudan) na RS Berkane (Morocco).

Katika hatua nyingine, CAF imetaja timu 10 zinazowania tuzo ya Timu Bora ya taifa ya Mwaka 2025 upande wa wanaume.

Timu hizo ni Morocco, timu ya taifa ya vijana ya Morocco chini ya umri wa miaka 20, Algeria, Cape Verde, Ivory Coast, Ghana, Afrika Kusini, Tunisia, Senegal na Misri.