Tuwapate kina Raila wengine | Mwananchi

Wiki ijayo tunakwenda kupiga kura kukamilisha Uchaguzi Mkuu wa nchi yetu. Tumeshuhudia kampeni za moto, vuguvugu na baridi katika kuelekea huko. Vipo vyama vilivyofanya kampeni za nguvu sana, vingine vilifanya kwa kuchechemea, na vilivyobaki havikufanya kabisa. Ya kusemwa yamesemwa na ya kusikilizwa yamesikilizwa, hatimaye sasa wananchi wapo tayari kwenda kituoni kuzungumza na boksi la kupigia kura.

Takwa la mpigakura yeyote ni kumpata kiongozi atakayemsikiliza na kumjali kwa ukaribu. Takwa hili wakati mwingine husababisha watu kuamini “watu wao” au “vyama vyao”. Pengine wanaweza kusahau kuchunguza matamanio yake, na akajikuta amechagua koroma badala ya nazi. Na kwa bahati mbaya maji yakishamwagika hayazoleki; vidole vikishatumbukiza karatasi kwenye boksi haviwezi kuirudisha karatasi hiyo mezani.

Kwenye kampeni, hakuna kiongozi anayeweza kuahidi kuwa akichaguliwa atakwenda kula rushwa. Kila mmoja atasikilizwa na kupigiwa kura kwa kadiri atakavyotumia ufundi wa maneno ya kujinadi. Uhalisia wake utakuja kuonekana baadaye wakati hakuna wa kumzuia ndani ya miaka mitano ya mwanzo, au miaka kumi ya kikatiba. Wakati huo ndio mpigakura atakapojua iwapo aliramba turufu au garasa.

Viongozi wazuri ni wale wanaoyaishi maneno yao. Kwenye hali yoyote, kiongozi anasimamia yale anayoyaamini bila kubadili gia. Ipo nadharia iliyotokana na hadithi ya kale iliyomhusu kijana kijana aliyekwenda kumfuata mchumba. Alipewa sharti la kwenda mbele bila kutishwa na sauti za mizimu. Na kwamba iwapo angetishika na kugeuka, sekunde hiyohiyo angebadilika na kugeuka jiwe.

Ni jukumu rahisi sana kwa nadharia. Kijana angejiambia: “Ishu ni kufika kileleni, nitakanyaga hapa, hapo na pale hadi nafika juu. Nikisikia shobo yoyote naipotezea”. Lakini mlima ule ulijawa na mawe yanayosemekana kuwa hapo mwanzoni, yalikuwa ni vijana waliotia nia kama yeye. Lakini walishindwa kuhimili vishindo, wakalazimika kukiuka masharti na kujikuta wakibadilishwa kuwa mawe.

Kiongozi yeyote ni binadamu mwenye wazazi, familia, ndugu, jamaa na marafiki.

 Utajisikiaje pale utakapofanikiwa kukaa kileleni, halafu ukaipoteza roho ya kipenzi wako kwa kushindwa kukiuka kipengele kimoja tu cha katiba uliyoiapia?

Kumbuka kuwa pembeni yako kuna sauti za wazazi, ndugu na familia zinazokulilia. Na hizi ndio mfano halisi wa sauti za vitisho za mlimani, au sauti za mizimu.

Pamoja na hayo, dunia ina watu walio tofauti na wengine.

Tumewazoea wale ambao wakisema “sitakula mpaka kieleweke,” lakini kesho wataamka wakiwa wamekula mkate kizani. Lakini wapo ambao wakisema “nyeusi” wanamaanisha nyeusi. Mmoja wao ni yule ambaye Wakenya wa itikadi zote walimwita Baba na Jogoo. Wengine walimfahamu kama “yule jamaa wa maandamano.” Huyu ni Raila Odinga.

Raila alikuwa mkosoaji mkubwa wa siasa za Kenya. Kama wote tunavyoelewa, siasa ni mchezo usio na huruma. Shujaa huyu alipitia figisu za kila aina kisiasa. Lakini nyuma ya kelele za siasa, kuna kitu kimoja kisichopingika kwake: uadilifu. Alikuwa ni mwarobaini uliotukanwa barabarani lakini ukabaki na tiba yake. Wale walioutukana waliurudia na kulazimika kuunywa baada ya kushindwana na tiba zingine.

Hakuna kizuri kinachokosa kasoro, na mtu yeyote anapimwa kutokana na mazuri na mabaya yake. Mzee huyu alikuwa na kasoro zake kama binadamu yeyote. Lakini ukiweka pembeni siasa, unakiri kwamba uadilifu wake ni kama kabati la babu; halina mlango wa siri. Anaongea hadharani, anapoteza hadharani, na akishindwa, bado anawapongeza washindi kwa tabasamu. Kisha anarudi kwenye harakati zake za kimaisha.

Kitu kikubwa kinachomtofautisha na wanasiasa wenzake, ni kuujali utaifa wao zaidi ya kitu kingine chochote. Kenya ni nchi yenye siasa za kikanda.

Lakini yeye pamoja na kuzaliwa kwenye familia yenye historia ya siasa na ukwasi wa mali, hakuitumia hiyo kama bakora kimaisha.

Hakuunga mkono siasa zilizowagawanya watu kwa vigezo vya kanda, badala yake aliwaongoza Wakenya kudai haki zao kwa pamoja.

Kwa jinsi alivyoipenda Kenya, alikuwa tayari kuacha biashara zake zikiendeshwa na watu wengine. Alikuwa radhi kuwahudumia wengine kwa manufaa ya nchi yao. Mara kadhaa amekuwa akiwasihi wafuasi wake waachane na mihemko na kutanguliza utaifa.

Mara zote wafuasi wake waliamini kuwa kiongozi wao alifanyiwa figisu katika chaguzi, lakini yeye aliwaambia kuwa aliyechaguliwa “anatosha”, na wauachie wakati utakapokuja kuongea. Kila nchi ina watu ambao wapo tayari kusimamia haki zao kwa njia yoyote; iwe kikatiba, kisheria na hata kimabavu.

Ni wachache sana kati yao wanaojua kuwa uadilifu ni uvumilivu kwa kuamini wakati.

Kwamba kama haki iko upande wako, jogoo awike au asiwike ni lazima kutakucha. Kwa hiyo ungemuona Raila akiketi kimya kwenye benchi la bunge au akicheka na watawala, ukadhani amechoka. Hapana, aliamini katika wakati.

Hivi sasa kila mmoja anaamini kuwa Kenya ingepata Rais wa aina ya Sam Nujoma kupitia Raila.

Lakini wakati umeshamuacha, hivyo wanahitaji mno kuwa na Raila mwingine. Kadhalika sisi, tunahitaji sana kuwa na kiongozi wa aina ya Raila Odinga. Hata kama atakuwa upande wa upinzani, lakini mwenye sifa ya kupigania utaifa kuliko utawala.