Mazungumzo ya nyumbani, yale ya kipindi cha chakula hususan cha jioni, kwa kiasi kikubwa ndiyo hujenga mitazamo ya familia na ‘kushepu’ ubongo wa watoto. Upendo au chuki, hasi au chanya za familia, kwa sehemu kubwa ni matokeo ya lugha ya mezani.
Tabia za watoto, ukarimu au uchoyo, kupenda kujumuika na wanajamii au kujitenga, kila kitu, kwa sehemu kubwa, chanzo chake ni aina ya mazungumzo ambayo wazazi huyafanya mezani.
Maisha ya dada wa kazi kuweka chakula mezani, kila mmoja anakula kwa wakati wake, hakuna makutano ya pamoja mezani, husababisha watoto au vijana kujikuza kwa namna yao pasipo kujengwa na wazazi. Utamaduni wa chakula cha pamoja mezani, huwajenga watoto kuwa wanafamilia bora. Huwafanya kugundua haraka nyakati za chini na juu za wazazi wao.
Huyatambua majira ya mvua na jua. Hujionea namna wazazi wao wanavyovikabili vipindi vyenye masononeko, hufurahi pamoja nao awamu za furaha. Hujifunza kujali na kubeba majukumu, kulingana na uhusika wa wazazi wao.
Tanzania, watoto ambao wazazi wao walitokana na Kizazi cha Ukimya ambacho kinahusu waliozaliwa mwaka 1925 mpaka 1945 na Baby Boomers (1946 mpaka 1964), wao walipata maambukizi mazuri ya hisia kuhusu maisha ya ukoloni na utamu wa ukombozi baada ya uhuru kamili kupatikana. Darasani walifundishwa na walimu wenye vionjo vya hali za maisha kabla na baada ya uhuru.
Majina wapigania uhuru, yalijadiliwa kwenye mabaraza ya soga na vijiweni, kisha nyumbani wakati wa chakula, halafu alikutana na walimu walioona na kujifunza mengi. Walimu waliopita Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wanaojua maana ya uzalendo, walifundisha misingi na umuhimu wa kulinda nchi.
Mtoto wa Kitanzania alikuwa akijua kwamba wajibu wake namba moja ni kuilinda na kuitetea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere liliimbwa na kujadiliwa kuanzia nyumbani, vibarazani, vijiweni na shuleni kuwa ni shujaa. Kila Mtanzania alijua kuwa Bibi Titi Mohamed ni mwanamke shujaa wa uhuru wa Tanganyika.
Mtoto wa Kitanzania alikuwa akijua kwamba Rashid Kawawa ni Simba wa Vita. Wazazi waliwalea watoto kuwa na mioyo mikubwa kwa taifa lao. Shuleni watoto waliimba “taifa litajengwa na wenye moyo.”
Naitazama Tanzania ile, naipitia ya sasa. Vijana wale na wa siku hizi. Tofauti haisemeki. Watoto wa Silent Generation na Baby Boomers, walikuwa na wasifu mzuri wa kimaadili. Walijua uongozi ni dhima inayobebwa na watu kwa jamii na nchi.
Walitambua umuhimu wa kuwaheshimu wabeba dhamana. Hawakuwa na uhodari wa kutukana viongozi, bali kuyaona makosa na kuyasema, kama ilivyo haki ya kidemokrasia.
Kizazi X (Generation X), ambacho ni waliozaliwa mwaka 1965 hadi 1980, halafu Millennials, ambao ni kizazi cha mwaka 1981 mpaka 1996, vizazi hivyo viwili, vina mchango mkubwa kwenye uwepo wa vijana wa sasa. Vijana mahiri katika matumizi ya mitandao ya kijamii. Athari ya kimtandao hivi sasa, aina ya maudhui yanayosambaa, moja kwa moja yanaakisi malezi ya X na Millennials.
Familia hazizungumzi, isipokuwa zinapishana. Muda wa chakula kila mtu ana simu mezani. Ni rahisi wanafamilia kujadili mpira na umbea wa mitandao, kuliko masuala ya nchi. Inapotokea habari kuhusu nchi zinazojadiliwa kwenye familia, zinakuwa zenye vyanzo vya mitandao. Zile zenye kupandikiza chuki na kukatisha tamaa. Fulani ni tajiri sana, anamiliki asilimia 50 ya maghorofa ya Dar es Salaam. Hapo mategemeo ni yapi?
Wazazi hawakai na watoto wao kuzungumza kuhusu mahali waliikuta nchi na walivyoshuhudia mabadiliko. Taifa ambalo miaka 20 iliyopita, ilikuwa barabara za vumbi nchi nzima. Leo, mikoa yote ya Tanzania inaunganishwa kwa lami. Kutoka treni (gari moshi) mpaka standard gauge.
Wazazi hawawasimulii watoto ajali ya treni ya Igandu na Msagali, kwa hiyo hawawezi kuziona hatua kubwa za SGR. Umeme leo hadi vijijini. Je, unapatikana muda wa kuthamini jitihada?
Tulioshuhudia ajali ya basi la Ally’s, Nyakato, Mwanza, watu wakiuawa mbele ya macho ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa, tuna nafasi ya kuwaambia watoto wetu kuwa nchi imetoka mbali. Inatakiwa kuendelea kupigania maendeleo na ustawi zaidi, huku wakitambua kwamba zipo jitihada za hali ya juu zilifanyika kuifanya Tanzania ifike mahali ilipo.
Rais hadi rais, Mwalimu Nyerere, kisha Ali Hassan Mwinyi, Mkapa hadi Jakaya Kikwete, Dk John Magufuli mpaka Rais Samia Suluhu Hassan, kila mmoja amekuwa na jitihada za kuisogeza nchi mbele. Inatakiwa kutambua mchango wa kila mmoja na kuuthamini, kama ni kukosoa, basi ukosoaji ujengwe katika muktadha unaotambua mema ya anayekosolewa.
Mitandaoni ukifuatilia maoni ya watu, hasa vijana wasiowajua viongozi, wanavyowazungumzia, utadhani ni ibilisi ambao hawajawahi kuwa na manufaa yoyote kwa nchi. Ukweli ni kuwa pamoja na athari ya mitandao, shida kubwa inaanzia ndani ya malezi. Usipomlea mwanao na kumjenga kuchanganua mambo kwa kutumia akili yake, atageuka mfuata mkumbo. Daima, anayefuata mkumbo bila kuishirikisha vizuri akili yake, anakuwa anapoteza utu wake. Hatofautiani na roboti.
Hii inahusu zaidi kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu 2025. Limebaki juma moja kufanyika kwa uchaguzi. Je, maudhui ya maongezi kwenye meza za chakula nini? Mjadala ni maendeleo, haki za kiraia na huduma za kijamii, au hamasa ya kuandamana kupinga uchaguzi? Je, wazazi wanapata wasaa wa kusimulia watoto wao kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan, Sudan Kusini, Libya na mataifa mengine?
Wazazi wanapaswa kufahamu, kisha wawaeleze watoto wao ambao ndiyo vijana wa sasa, kuwa taifa kutumbukia kwenye machafuko ni rahisi, ila amani kurejea huwa kazi ngumu ajabu. Misuguano ipo, hilo halina ubishi, Uchaguzi Mkuu umewadia, na ni vigumu kuuzia kufanyika. Vema hamasa iwe maridhiano na mwafaka baada ya uchaguzi. Msisitizo iwe kutimia kwa ahadi ya kupatikana Katiba Mpya, kama ilivyotolewa na Rais Samia.