Wakulima wa mwani Mtama wapatiwa vitendea kazi

Mtama. Katika kuboresha zao la mwani nchini Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wametoa vitendea kazi kwa wakulima wa zao hilo, kwenye Halmshauri ya Mtama, mkoani Lindi.

Vifaa hivyo vimetolewa kupitia ofisi ya Waziri mkuu (Sera, Bunge na uratibu) kwa kushirikiana na wadau kutoka Agriculture and Fisheries Development Program (AFDP), ambapo wametoa vifaa vyenye thamani ya Sh179 milioni kwa wakulima wa mwani kutoka kijiji cha shuka kata ya Navanga ,Halmashauri ya Mtama.

Akizungumza na wakulima wa zao la mwani leo Jumatano Oktoba 22,2025 Mkuu wa Wilaya ya Lindi,  Victoria Mwanziva amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kukuza zao hilo.

“Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wakulima wa mwani pamoja na kuwafundisha matumizi bora ya vifaa vya kisasa, lakini pia tutashirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza zao hili la mwani kwani linaleta kipato katika mkoa wetu na Taifa kiujumla,”amesema Mwanziva.

Aidha Mratibu wa mradi kutoka AFDP, Salim Mwijaga amesema kuwa AFDP imekuwa ikitekeleza miradi ya kuwawezesha wananchi katika sekta ya kilimo na uvuvi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mwijaga ameendelea kusema kuwa katika ushirikiano na Serikali wametoa vifaa vya kisasa kwa wakulima wa mwani katika vijiji vinne vya Shuka, Mmongomongo, Mnumbu na Sudi.

“Tumetoa vifaa vya boti, viatu, kamba kubwa na dogo, kofia za usalama na glovu, lengo ni kuboresha shughuli za kilimo cha mwani na kuongeza tija kwa wakulima.”

Hadija Sudi mkulima wa mwani kutoka kijiji cha Shuka amewashukuru wadau na Serikali katika kusaidia kuwapatia vifaa hivyo vya kisasa kwani watakwenda kuzalisha kisasa zaidi kuliko awali.