Watu 14 Wafariki, Ajali ya Treni Ethiopia – Global Publishers



Watu 14 wamefariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa baada ya treni ya abiria kupata ajali mapema Jumanne katika njia ya reli ya Dire Dawa Dewele mashariki mwa Ethiopia, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali za mitaa nchini humo.

Ajali hiyo ilitokea saa 8 usiku wakati treni hiyo ilikuwa ikisafiri umbali wa takriban kilomita 200 kutoka mji wa Dewele, ulioko karibu na mpaka wa Djibouti.

Picha zilizochapishwa na Dire TV zilionyesha mabehewa kadhaa yakiwa yamepinduka na mengine yakiwa yameharibika vibaya. Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu chanzo cha ajali hiyo.

Uchunguzi umeanzishwa ili kubaini chanzo cha ajali hiyo, huku maafisa wakikagua upya hatua za usalama katika mtandao mzima wa reli nchini.