Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha Ada Tadea, Juma Ali Khatib amesema akichaguliwa kuwa Rais ataimarisha Mji wa Wete kuwa kituo cha biashara kwa kujenga bandari itakayowezesha meli kubwa za mizigo kufunga gati moja kwa moja katika bandari hiyo.
Mgombea huyo ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 23, 2025, alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Jadida, Wilaya ya Wete, mkoani Kaskazini Pemba.
Amesema katika kuinua Mji wa Wete kibiashara, ni lazima kuwepo na bandari yenye uwezo wa kuziwezesha meli kubwa za mizigo kutoka nje kutua bandarini hapo.
Amesema hatua hiyo itasaidia kufunguka kwa mji huo, kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, jambo litakaloongeza ajira kwa vijana na kukuza kipato chao.
“Mtakaponichagua, nitaufanya Mji wa Wete kuwa mji wa biashara kwa kuimarisha miundombinu ya bandari kwa ujenzi wa bandari itakayoziwezesha meli kubwa za mizigo kufika bandarini hapo,” amesema Juma.
Amesema hatua hiyo pia itasaidia kuwapa unafuu wa maisha wananchi wa maeneo hayo, pamoja na kupunguza bei za bidhaa zitakazoingizwa nchini.
Aidha, amesema mbali na kuimarisha miundombinu ya bandari, Serikali yake itawaangalia vijana kwa kuwapatia fedha za kununua bodaboda na bajaji ili kujiendesha kiuchumi.
Ameeleza kuwa atawainua wajasiriamali wanawake kwa kuwapatia mitaji itakayowawezesha kuongeza kipato chao na kuondokana na umaskini.
Awali, akizungumza katika kampeni za chama hicho, Haitham Nassor Suleiman amesema iwapo wananchi watakipa ridhaa chama hicho kuingia madarakani, kitaelekeza nguvu zake kwa vijana kwa kutoa ajira 500,000 ili kuondoa changamoto ya ajira kwa vijana.
Amefafanua kuwa mara nyingi vijana wamekuwa wakihangaika kutafuta kazi, hivyo watakapoingia madarakani watawaangalia kwa karibu vijana.
“Mtakapokiwezesha chama chetu kuingia madarakani, tutaelekeza nguvu zetu kwa vijana kwa kutoa ajira 500,000 ili kuondoa changamoto ya ajira kwa vijana,” amesema.
Kwa upande wake, mweka hazina wa chama hicho, Ali Mohamed Ali amesema Ada Tadea kitajikita katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara.
Amesema katika ujenzi wa miradi ya barabara, nyumba zitakazoathirika na miradi hiyo watahakikisha wanawajengea wahusika nyumba nyingine, na kama ni mimea ikiwemo mikarafuu, watalipa fidia kwa shina moja kwa Sh500,000.
Hata hivyo, amesema katika Serikali yao, watasamehe tozo za bodaboda na bajaji ili kuwapa nafasi ya kufanya kazi zao kwa urahisi.
