Dar/mikoani. Ajali ya treni ya SGR iliyotokea mapema leo katika kituo cha Ruvu mkoani Pwani, mbali na kukwamisha safari za abiria kwa muda, imeacha maswali lukuki kuhusu chanzo chake.
Treni hiyo iliyokuwa ikitokea jijini Dar es Salaam, imehama njia kufuatia kile ambacho Shirika la Reli Tanzania (TRC) limekitaja “sababu za kiuendeshaji” kuwa ndiyo chanzo cha ajali hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Shiwa alipotakiwa kufafanua, amesema ni hitilafu zinazoweza kusababishwa na mtu au kifaa, lakini si kutokana na miundombinu ya reli.
Machibya amesema hayo alipo alipohojiwa na Mwananchi kuhusu ajali hiyo na hatua zilizoanza kuchukuliwa.
“Kuna changamoto ilijitokeza kwenye uendeshaji, haihusiani na njia. Miundombinu ya reli ilikuwa imara isipokuwa changamoto iliyotokea kwenye uendeshaji ndiyo ilianzisha hili tatizo. Na ndiyo maana tumeweza kurejesha huduma haraka kwa kuwa miundombinu haikuwa na changamoto, ijapokuwa treni imeathirika kutokana na hilo tatizo la kiuendeshaji,” amefafanua.
Hata hivyo, ufafanuzi huo umeibua maswali ya wadau kupitia mitandao ya kijamii wakihoji kama hitilafu imesababishwa na mtu ni nani na amechukuliwa hatua gani? Kama ni kifaa ni kipi, kimeharibika lini na nani anawajibika kukirekesha? Na je, kwa nini taarifa ya shirika isieleze jibu moja ama ni kifaa au ni mtu?
Hata hivyo, licha ya maswali hayo kukosa majibu, taarifa mbalimbali kuhusu ajali za treni dunia, zinataja mambo mbalimbali yasababishayo kama ajali hizo, yakiwemo makosa ya binadamu kama chanzo kikuu.
Kufuatia ajali hiyo iliyotokea dakika 25 tangu treni hiyo, maarufu kama mchongoko kuondoka jijini Dar es Salaam saa 2:00 asubuhi, Oktoba 23, 2025 safari za SGR zilisitishwa kwa muda na kuwalazimu mamia ya abiria kusubiri kwa muda usiojulikana.
Abiria aliyekuwa katika Stesheni ya Magufuli Dar es Salaam, amesema: “Kwa kuwa hakuna maelezo yaliyonyooka kama tutaondoka au la, nimeamua kwenda uwanja wa ndege kwa sababu nina kikao saa tisa alasiri na nimekuja hapa tangu saa mbili asubuhi, lakini hadi saa sita mchana sioni mwelekeo wa kile walichoeleza,” amesema Anastazia Njenge.
Abiria mwingine, kutoka Ujerumani aliyejitambulisha kwa jina la Johannes Muller, alisema wameamua kurudi hotelini kusubiri taarifa zaidi.
Hata hivyo, Mwananchi ilipofika katika Stesheni ya Magufuli imeshuhudia baadhi ya abiria wakiendelea kuondoka huku wengine wakisubiri taarifa zaidi.
Wakati huohuo, abiria wengine walikuwa wanafika stesheni hapo wakitaka kupata uhakika wa safari za leo baada ya kuona taarifa mitandaoni kuhusu ajali hiyo.
Katika Stesheni ya Jakaya Kikwete mjini Morogoro, abiria waliokuwa wakisubiri usafiri wa treni ya SGR kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam walilazimika kuahirisha safari zao.
“Wakati nafika tayari nilishakuwa na taarifa za kuwepo wa ajali hi,i lakini niliona nisubiri taarifa kamili kutoka kwa mamlaka husika, sasa baada ya kufika hapa ndio nikasikia tangazo likituomba tuhairishe safari kwa sababu treni iliyopita ajali imeziba njia,” amesema Omary Mrisho.
Naye Yusta Komba amesema alipanga kusafiri na treni ya SGR ya saa 5:50 na aliamini angefika Dar es Salaam mapema na kupata muda wa kupumzika kabla ya kwenda kwenye sherehe ya kumuaga binti yake, jana jioni.
Zaidi ya abiria 800 pia walikwama kwa muda katika stendi ya treni ya mwendo kasi (SGR) kituo cha Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma.
Mmoja wa abiria waliokuwa wakielekea Dar es Salaam, Aisha Nurudin Saidi, amesema kuwa taarifa ya ajali waliisikia mapema kupitia mitandao ya kijamii, lakini hawakupata taarifa rasmi kutoka mamlaka husika.
Baada ya kukwama hadi mchana, baadaye safari zilirejea kama kawaida, kwa mujibu wa taarifa ya TRC.
Akielezea kurejea kwa safari za treni jana alasiri, Machibya alisema treni ya saa 8:10 mchana kutoka Dodoma na ya Morogoro zilikuwa zimeanza safari, Huku iliyokuwa Ruvu nayo ikishaondoka kwenda Dodoma.
“Safari haziwezi kuathirika ziko vilevile, zilizoathirika ni mbili ya Morogoro kuja Dar es Saalaam na ya saa 3:30 kuelekea Dodoma, hizo ndiyo zimeathirika. Zingine zote zitaendelea na huduma kama kawaida,” amesema.
Katika ajali hiyo hakukuwa na madhara zaidi kwa binadamu, isipokuwa taharuki kwa waliokuwa ndani ya treni hiyo.
“Ulikuwa ni mshtuko tu, hatujamuona mtu aliyejeruhiwa,” amesema mmoja wa abiria waliokuwa safarini.
Hii ni ajali ya kwanza kutokea tangu kuanza kwa huduma ya reli ya kisasa nchini Tanzania, Juni 14, 2024, ingawa zimekuwepo hitalafu kadhaa za kiufundi.
Septemba 9, 2024 treni hiyo ya SGR iliyokuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ilipata hitilafu ya kiufundi na kukwama Ngerengere kwa zaidi ya saa tatu huku abiria waliotakiwa kusafiri saa 12 jioni kwenda Dodoma wakikaa stesheni kwa zaidi ya saa 5 bila taarifa yoyote.
Julai 30, 2024 hitilafu ya umeme iliyojitokeza kati ya Stesheni ya Kilosa na Kidete na kusababisha treni kusimama kwa muda wa saa mbili njiani, ngedere na bundi wakitajwa kuwa chanzo cha uharibifu.
Usiku wa Alhamisi, Agosti mosi, 2024 SGR kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam ilikwama kwa muda mkoani Morogoro. Treni hiyo ilikuwa imebeba abiria na wageni mbalimbali waliotoka kwenye uzinduzi wa huduma za SGR zilizofanyika mkoani Dodoma.
Ukiacha matukio hayo ya kiufundi, tangu huduma za SGR zizinduliwe treni imekuwa ikifanya safari zake bila tatizo kubwa.
Ingawa kila ajali ni ya kipekee, mtandao wa shinerlawgroup.com unataja sababu kuu za ajali za treni za umeme kuwa ni makosa ya kibinadamu kama uzembe wa kondakta wa treni, mhandisi, au watu wanaofanya kazi kwenye reli.
Mambo mengine nio waendesha magari au watembea kwa miguu wasio waangalifu, hitilafu za kifundi, uendeshaji kasi kupita hali halisi ya mazingira, ubovu au kasoro kwenye reli, treni kupinduka, vituo au vivuko vya reli visivyolindwa na vitendo vya watu kujiua.
Changamoto za kawaida ni pamoja na reli kuvunjika au kupinda, swichi kuwa hitilafu, hitilafu kwenye mfumo wa breki, kupuuza ishara na matatizo ya kimazingira kama hali mbaya ya hewa, vizuizi kwenye reli na treni kukongana.
Kwa mujibu wa Takwimu za Shirika la Usafiri (Bureau of Transportation Statistics), kwa wastani kuna takribani ajali 1,800 za treni kila mwaka duniani, nyingi kati ya hizo zikiwa na majeruhi wengi na wastani wa vifo vitano hadi saba kwa mwaka.
Mfano, mwaka 2019 kulikuwa na ajali 1,848 za treni, zikiwemo 1,283 zilizopinduka na 115 zilizogongana na 450 zilizoorodheshwa kama ajali za aina nyingine. Ajali hizo zilisababisha majeruhi 57 na vifo vinne.
Mwaka uliotangulia, 2018, kulikuwa na ajali 1,934 za treni, zikiwemo 1,375 za kupinduka na 86 za kugongana, 473 zilizoorodheshwa kama ajali nyingine. Ajali hizo zilisababisha majeruhi 204 na vifo saba.
Imeandaliwa na Hamis Mniha na Rachel Chibwete (Dom) Hamida Sharif (Morogoro) Devotha Kihwelo na Herieth Makwetta (Dar