Andabwile asiiangushe Yanga na Folz

YANGA ilipoamua kumsajili Aziz Andabwile kutoka Singida Fountain Gate kuna kitu ambacho ilikiona kwa mchezaji huyo na ikaamini atatoa mchango kwenye kikosi chake.

Sisi hapa kijiweni tunaamini hizi timu zetu kubwa hapa nchini huwa hazisajili mchezaji mzawa ambaye hazijaona kitu ndani yake maana hawa wa kwetu ni rahisi kuwafuatilia ndani na nje ya uwanja.

Na hicho kitu cha Andabwile kikaja kuonekana pindi Yanga ilipokuwa chini ya kocha Mfaransa Romain Folz ambaye kibarua chake ndani ya timu hiyo hakijawa cha muda mrefu baada ya mkataba wake kuvunjwa hivi karibuni kutokana na kiwango kisichovutia.

Yanga wengi hawakumuelewa Folz lakini sidhani kama kuna mtu ambaye alikuwa akinufaika na uwepo wa kocha huyo kumzidi Aziz Andabwile ambaye kabla yake hakuwa akipata nafasi ya kutosha ya kucheza.

Folz alimuamini Andabwile akampa nafasi ya kucheza tena hadi katika mechi ngumu kama dhidi ya Simba jambo ambalo lilizidi kumjengea hali ya kujiamini kiungo huyo wa zamani wa Mbeya Citu na hivyo watu wakaanza kuona kile alichonacho.

Sasa Folz anaondoka na kijiwe kinaamini kwamba anaacha mtihani mgumu kwa Andabwile ambaye anatakiwa kuupa majibu au kufeli kutegemeana na kitakachotokea chini ya utawala wa kocha mpya.

Mtihani huo ni kuonyesha kuwa hakupata nafasi ya kucheza chini ya Folz kwa bahati ya mtende bali ni uwezo na kiwango chake bora kuanzia mazoezini na katika mechi.

Ili Andabwile aufaulu mtihani huu anatakiwa kuondoa unyonge wa kuondoka kwa Folz. Aendelee kuamini kwamba alipewa nafasi ya kucheza kwa kustahili jambo ambalo pia linaweza kumshawishi kocha mpya kumpa nafasi.

Kama akijitia unyonge itamuathiri kisaikolojia na hivyo atashindwa kutoa kiwango bora jambo ambalo litamfanya apoteze nafasi ya kucheza kikosini.