Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimehoji mahali alipo Makamu Mwenyekiti wake Bara, John Heche aliyekamatwa na Jeshi la Polisi katika viunga vya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, jana Oktoba 22, 2025.
Chadema kupitia taarifa yake kwa umma iliyoitoa leo Oktoba 23, 2025 na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, imelitaka Jeshi la Polisi kutoa taarifa ya wapi alipo kiongozi huyo.
“Leo asubuhi timu ya mawakili pamoja na viongozi wa Chadema imefika kituo cha Polisi Tarime kufuatilia taarifa za kukamatwa kwa Makamu Mwenyekiti Taifa.
“Timu yetu imeelekezwa na Polisi Tarime iende Ofisi ya Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Tarime ambapo ilipofika ikaambiwa kuwa ofisi hiyo haijui lolote kuhusu kukamatwa na kusafirishwa kwa Heche,” taarifa hiyo imeeleza.
Kutokana na hali hiyo, timu ya Chadema ilifika kituo cha Polisi Musoma kupata taarifa za makamu wao na kuambiwa hawana taarifa hizo.
Pia, chama hicho kinaeleza kuwa kilimtafuta Msemaji wa Idara ya Mawasiliano, makao makuu, lakini simu zake hazikupokelewa.
Chama hicho kimemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camilius Wambura kutoa maelezo ya haraka ya wazi na yenye ukweli kamili juu ya mahali alipo Heche.
“Tunasisitiza usalama wa raia hauwezi kuwa kwa maneno bali kwa vitendo, kumficha kiongozi wa kisiasa ni uvunjaji wa haki za msingi za binadamu na ni dalili za kuendelea kuzorota kwa utawala wa sheria nchini,” amesema.
Mwananchi ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pius Lutumo, kama kiongozi huyo wa Chadema kapelekwa Mara amesema hana taarifa hizo na Mara ina mikoa miwili.