Dk Mwinyi afunga kampeni Pemba akitaja dhamira ya CCM kulinda tunu za Taifa

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amefunga kampeni kisiwani Pemba akitaja mambo watakayoyaendeleza ikiwa ni pamoja na maridhiano na kudumisha amani.

Amewataka wananchi wasibweteke badala yake wajitokeze kwa wingi kukupigia kura chama hicho ili kuendeleza tunu za Taifa, ikiwemo amani, umoja na mshikamano kwa madai kuwa hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuendeleza vitu hivyo.

Amesema kama wanataka kuendeleza Muungano, amani na mshikamano wakichague chama hicho kwani ndio chama pekee chenye dhamira ya kulinda tunu za taifa.

Wakati akizungumza na wananchi, wanachama na wapenzi wa chama hicho leo Oktoba 23, 2025 katika uwanja wa Shaame Jimbo la Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dk Mwinyi amesema katika kipindi chote cha kampeni wameeleza dhamira yao ya kuhakikisha wanalinda umoja, mshikamano na maridhiano.

Wananchi, wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi wakiwa Kwenye mkutano wa kufunga kampeni za chama hicho kwa nafasi ya urais katika uwanja wa Shame Mattar Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba

“Leo tunafunga kampeni lakini tunakwenda kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba, niwatake tusibweteke siku ikifika tujitokeze kuchagua CCM ili kuendeleza tunu za Taifa,” amesema Dk Mwinyi.

Dk Mwinyi amewataka wananchi wasiwe na hofu kwani wamejipanga kuhakikisha usalama wa kutosha siku hiyo.

“Ndugu zangu tumefanya kampeni zetu kwa takribani siku 61, katika kampeni zetu tumehubiri amani, upendo, mshikamano na maridhiano, maana tunasema bila amani hata haya tunayoyataka kufanya itakuwa kazi bure,” amesema.

Licha ya kusema wamefanya kampeni kwa siku 61, hata hivyo kwa upande wa Zanzibar kampeni zimefanyika kwa takribani siku 46.

Amesema wataendelea kuhubiri amani na umoja ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana.

Kuhusu sekta ambazo watazizingatia wakirejea madarakani, Dk Mwinyi amesema wataendelea na ujenzi wa miundombinu ya ujenzi wa viwanja vya ndege, kutengeneza barabara na kujenga bandari za Mkoani, Wete na Shumba kwa mikoa ya Pemba.

Wananchi, wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi wakiwa Kwenye mkutano wa kufunga kampeni za chama hicho kwa nafasi ya urais katika uwanja wa Shame Mattar Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba

“Katika huduma za jamii, tutajikita katika kuboresha elimu, maji na kujenga hospitali za mikoa,” amesema.

Kwenye elimu, amesema wataendelea kujenga shule za kisasa na kuajiri walimu bila kusahau kuboresha mishahara yao.

Kwa upande wa maji, Dk Mwinyi amesema katika kipindi kinachokuja, watahakikisha hakuna tatizo la maji katika maeneo yote ya Zanzibar ambapo kwa sasa tayari wameanza kujenga matanki makubwa ya maji.

“Kwenye afya tutajenga hospitali za mikoa na tutaanzia kujenga katika mikoa hii miwili ya Pemba, lengo ni kuhakikisha watu wanapata huduma za afya katika

Akizungumzia kuhusu uchumi wa buluu, mgombea huyo amesema wataendelea kuwa sekta mama kutokana na umuhimu wake na kubeba sekta nyingi ndani yake ukiwemo utalii, uvuzi, mafuta na gesi, usafirishaji baharini.

“Tukipata mafuta na gesi, huu ni uchumi mkubwa sana, kwa hiyo tukianza kuchimba tutapata uchumi mzuri.

Kuhusu usafiri baharini, amesema unakwenda kupata mwarobaini kwani kuna boti mpya za kisasa zipo mbioni kukamilika huku meli kubwa ya Mv Mapinduzi II ambayo nayo inatarajiwa kuanza kazi.

Amesema wana dhamira kujenga viwanda ili kusaidia vijana wengi wapate ajira katika sekta binafsi

Amesema watajenga viwanda vya kuchakata samaki, mwani na dagaa ili kuhakikisha mazao hayo ya bahari yanaendelea kuleta tija na kuongeza uchumi.

Awali, akimnadi mgombea huyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa amesema Dk Mwinyi ana upendo kwa wananchi wake na kati ya wagombea 11 ndiye pekee mwenye uwezo na mwadilifu akiwa na hofu ya Mungu.

Amesema anachukia rushwa na yupo tayari kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Amesema Dk Mwinyi amejitahidi kuondoa umaskini, maradhi kwa kujenga hospitali kubwa na kuondoa ujinga kwa kujenga shule nyingi ambapo wanafunzi kwa sasa wanaingia katika mkondo mmoja.