Dk Mwinyi: Tunataka kurejesha heshima ya zao la karafuu

Pemba. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesema Serikali imefanya uamuzi wa makusudi kukabidhi hatimiliki kwa wakulima wa karafuu ili kuyamiliki mashamba hayo kisheria na kuwawezesha kuyahudumia vizuri, wazalishe kwa tija.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 23, 2025, katika hafla ya ugawaji wa hati za mashamba ya Serikali, hasa ya karafuu, Mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema hati hizo zitawawezesha vizazi vyao kurithi mashamba hayo, kuyatunza, kupanda mipya, kuyahudumia, kumwagilia na kuhakikisha kiwango cha uzalishaji kinaongezeka ili kupata manufaa ya zao hilo muhimu kwa uchumi wa nchi na wakulima.

β€œSerikali inatambua mchango wa zao hilo kwa uchumi wa nchi na wakulima, hivyo ilikaa na kutafakari changamoto zinazokabili zao hilo na kugundua zipo changamoto nyingi ambazo zinasababisha uzalishaji wa karafuu kuwa wa chini,” amesema.

Dk Mwinyi amesema uzalishaji wa karafuu sasa hauzidi tani 10,000 kwa mwaka, na inapokuwa msimu mzuri hufikia tani 8,000, hali ambayo haitoi tija ya kutosha.

Amesema karafuu za Zanzibar ndizo bora zaidi duniani kwa kuwa na ubora wa hali ya juu.

β€œWapo wenzetu wanaochukua karafuu za nchi nyingine zenye ubora hafifu, halafu wanachanganya na za Zanzibar ili kuongeza ubora. Hivyo, tuna nafasi nzuri ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwani lina kiwango kizuri cha ubora,” amesema.

Rais Mwinyi amesema Indonesia huzalisha zaidi ya tani 100,000, jambo linaloleta swali kwa nini Zanzibar yenye karafuu bora zaidi inashindwa kufika hata tani 10,000.

β€œTuliangalia changamoto zilizopo na kugundua moja ni umiliki. Mashamba yakibaki chini ya umiliki wa Serikali, wananchi wanashindwa kuyahudumia vizuri. Ikifika msimu, mtu anaambiwa tumeshakodisha kwa fulani, hali inayomkatisha tamaa,” amesema.

Changamoto nyingine, amesema, ni kutokuwepo kwa kilimo cha kisasa, kwani mikarafuu mingi ni ya kurithi na mipya ni michache, hivyo Serikali imeamua kupitia Shirika la Biashara Zanzibar (ZSTC) kutoa miche bora bila malipo, kuhakikisha inatosha na ina ubora unaohitajika, sambamba na kuwawezesha wakulima kumwagilia bila kusubiri msimu wa mvua.

β€œTuna kila sababu ya kuwawezesha wakulima wamwagilie ili miche yote tunayopanda iweze kukua,” amesema.

Dk Mwinyi amesema hatua nyingine ni kuwepo kwa huduma za ugani kupitia mabwana na mabibi shamba wanaowafundisha wakulima mbinu bora za upandaji, upaliliaji na uvunaji, pamoja na kuwapatia mikopo ili waweze kutekeleza kwa vitendo mafunzo wanayopewa.

β€œTumepanga kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuwawezesha wakulima wa mikarafuu kupata mikopo isiyo na riba ili kuyaendeleza mashamba yao. Tukifanya hivyo, tutaongeza kiwango cha uzalishaji, jambo litakalosaidia uchumi wetu na kuwaondoa wakulima kwenye umaskini,” amebainisha.

Amesema katika kuongeza thamani ya zao hilo, elimu zaidi inahitajika kwa wakulima kuhusu namna bora ya kuhifadhi karafuu baada ya kuvuna ili kudumisha ubora unaotakiwa na kupata haki katika utambuzi wa ubora wakati wa kuuza.

Akizungumzia soko la zao hilo, amesema Serikali kupitia sera yake imeamua kwamba mkulima apewe asilimia 80 ya bei ya dunia.

β€œHili ndugu zangu, watu watakuja kuwaambia vinginevyo. Nataka niwapeni uhakika leo, sisi tukipata dola 10 huko tunapouza, hapa Zanzibar asilimia 80 ya bei hiyo anapewa mkulima, ambayo ni Dola nane.

β€œDola mbili zinazobaki zinatumika kugharamia huduma kama ununuzi wa magunia, uchukuzi na uendeshaji wa shirika. Wapo watu wanaokuja na kusema mnadhulumiwa, lakini nakupeni uhakika hakuna kitu cha siri. Ingieni mtandaoni mtaona bei ya karafuu mwaka huu,” amesema.

Rais Mwinyi amesema wakiruhusu soko huria, wafanyabiashara wataungana kushusha bei ili mkulima apate kidogo na wao kupata zaidi.

Amewaasa wakulima kuwa mfumo wa asilimia 80 una maslahi makubwa kwao, kwani Serikali haitazami kumpa mkulima bei gani, bali huangalia bei ya mauzo duniani ili kuhakikisha mkulima anapata asilimia 80 ya bei hiyo.

Ameahidi kuwa Serikali itaendelea na sera hiyo ya kutoa asilimia 80 ya bei ya kuuza kwa wakulima ili wanufaike na zao hilo.

β€œHaya yote ni kuona tunaongeza uzalishaji ili karafuu yetu iweze kuchangia katika uchumi wa taifa,” amesema.

Naye, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali, amewaomba wakulima kushirikiana na wizara, kwani hatua hiyo inahitaji ushirikiano na ukweli, huku akisisitiza kuwa Serikali haina nia ya kumdhulumu mtu.

Akitoa taarifa kuhusu ugawaji wa mashamba hayo, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi Zanzibar, Mussa Kombo Bakar, amesema hati hizo zinaipa ithibati na nguvu kwa wakulima kusimamia mashamba yao.

β€œInawezekana taratibu tunazozifanya zikawa zimesababisha baadhi ya wananchi kudhulumiwa, mashamba ya mirathi kuonekana ni ya Serikali. Ndio maana tumewashirikisha wakfu kuhakikisha haki za wananchi hazipotei, kilicho cha Serikali kibaki na cha wananchi kipate wenyewe,” amesema.

Amesema katika ugawaji wa hati hizo, zimetolewa hati 21 katika hafla hiyo, lakini wataendelea kutoa nyingine hadi kufikia mashamba 8,215 yaliyopo katika Kisiwa cha Pemba.

Sambamba na hayo, amesema wanatambua mchango mkubwa wa zao la karafuu na kuhakikisha mashamba hayo yanapata umiliki uliokamilika ili yasimamiwe vizuri zaidi.

Kwa mujibu wa Bakar, awali usimamizi wa mashamba hayo ulikuwa ukilegea kutokana na wananchi kukosa ithibati, lakini sasa Serikali itaendelea kutoa hati hadi shamba la mwisho ili wananchi waweze kuyasimamia ipasavyo.

β€œIla kuna changamoto kubwa imebainika wananchi wengi wanajenga kwenye maeneo ya kilimo. Tunaomba masheha wasimamie jambo hili,” amesema.