DK.SAMIA AWATAKA VIJANA KUIPENDA NCHI YAO,WASIKUBALI KUDANGANYWA KUIHARIBU

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa rai kwa vijana nchini wasikubali kudanganyika ili kuchafua amani ya nchi.

Akizungumza leo katika viwanja vya TANESCO -Buza villivyopo Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam akihitimisha mikutano yake ya kampeni za uchaguzi mkuu, Dk. Samia ametumia nafasi kuwaeleza vijana umuhimu wa kutunza amani iliyopo nchini.

Amesisitiza kwamba Tanzania ni eneo sahihi kwa vijana kuishi tofauti na maeneo mengine Afrika, hivyo amewataka wasikubali kufanganywa kwa namna yeyote ili kuvuruga amani ya nchi yao.

“Hapa mpo kwenye nchi yenye jina, yenye sifa zake, yenye kuendeleza watu wake. Msidanganywe wale ambao wapo nje wasiwadanganye. 

“Hapa mpo pazuri kweli kweli.Niwahakikishie vijana wa Tanzania, hawa wazee wenzangu wanaelewa. Vijana wa Kitanzania msidanganywe, ukichukua Afrika Mashariki, Kusini na Kati, Tanzania ni pepo.Nchi yetu iko salama”

Akisisitiza zaidi Mgombea Urais Dk.Samia amesema “Mkipata fursa kuingia kwa majirani zetu, mtaona vijana wenzenu wanavyokula ngumu. Mtasema mnataka kurudi kwenu.”

Amewakumbusha kuwa vijana ndio wanategemewa kukabidhiwa nchi kuiendesha kama inavyoendeshwa bila kudanganywa.”Katika kuongoza nchi, taifa limeweka mifumo mizuri ya kidemokrasia kwa kuchaguana kila baada ya miaka mitano.”

“Tulizeni munkali, nchi hii ni mali yenu, hakuna mwenye cheti anayesema nchii hii ni mali yangu. Sisi tunawakilisha wananchi, wananchi ndiyo nyinyi.Hakuna mwenye miliki ya wananchi, wananchi ndiyo nyinyi. 

“Tumepeana tu majukumu, niwaombe sana vijana msiharibu nchi yenu. Fuateni serikali yenu inavyowaambia, fuateni katiba yenu inavyowaelekeza,” amesema Dk.Samia.

Pamoja na hayo ametoa mwito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kupigakura kwani ndiyo haki ya msingi kidemokrasi.

“Hakuna mfumo uliowekwa kuhusu siasa safi kwani siasa safi ni kuhakikisha nchi na wananchi wapo salama ikiwemo kujumuishwa katika maamuzi.

“Serikali imekuwa ikiunda kamati kukusanya maoni kuhusu masuala mbalimbali yenye kuhusu maendeleo ya nchi.Hata panapotokea mazonge kwenye nchi tunaunda tume kuja kuwauliza, mnatoa maoni yenu. Hiyo ndiyo siasa safi.”

Ameongeza kuwa “Mnapokerana mnaitana kuzungumza, tuyazungumze, tuelewane, twende pamoja hiyo ndiyo siasa safi.”Amesema Dk.Samia na kuongeza  hayo ndiyo mambo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliyokuwa akiyasimamia ambapo serikali zote za CCM zimekuwa zikitekeleza.