Exim yakarabati jengo la watoto na vijana Muhimbili

Dar es Salaam. Benki ya Exim Tanzania imekabidhi jengo lililokarabatiwa la Kitengo cha Afya ya Akili kwa Watoto na Vijana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ikiwa ni jitihada za kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kuunga mkono ustawi wa afya ya akili nchini.

Ukarabati huo uliofanywa chini ya mpango wa uwekezaji wa kijamii wa ‘Exim Cares,’ ni sehemu ya kuimarisha mifumo ya afya nchini kwa kuunda mazingira salama, jumuishi na ya heshima kwa makundi yaliyo hatarini, hasa watoto na vijana wanaokabiliana na changamoto za afya ya akili.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa hafla ya makabidhiano, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim, Shani Kinswaga amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za muda mrefu za benki kuleta mabadiliko chanya ya jamii kupitia uwekezaji endelevu katika afya na ustawi wa jamii.

“Benki ya Exim siyo tu benki inayotoa huduma za fedha, bali pia ni sehemu ya mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii, tumeelekeza hatua zetu za kwanza katika afya ya akili. Tunaamini kuwa, afya ya akili si tu suala la matibabu, bali ni kipaumbele cha jamii na uchumi.

“Kitengo hiki kilichokarabatiwa hakioneshi tu miundombinu, bali pia ni mwakilishi wa dhamira yetu ya pamoja ya kujenga matumaini na heshima kwa kizazi kijacho,” amesema Kinswaga.

“Kupitia Exim Cares, tumeahidi kukusanya jumla ya shilingi milioni 300 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kampeni za uhamasishaji wa afya ya akili kote nchini. ushirikiano wetu na Muhimbili ni sehemu ya maono haya mapana ya kuhakikisha huduma za afya ya akili zinapatikana kwa urahisi, zinatolewa kwa ufanisi na kwa ukarimu.”

Kinswaga ametaja mchango wa washirika wa sekta ya bima kama vile Alliance General, Strategis General, Heritage Insurance Co, Alliance Life na MUA, ambao wameungana na Benki ya Exim kupitia Tamasha la Bima Amsha Matumaini.

Kampeni hizo zinalenga kuhamasisha jamii, kupambana na unyanyapaa na kukusanya rasilimali kwa ajili ya msaada na huduma za afya ya akili.

“Ushirikiano wetu na washirika kutoka sekta ya bima, ni kielelezo thabiti cha kile kinachoweza kufanikishwa kupitia ushirikiano wa sekta binafsi na umma pale wanapounga mkono na kua na nia njema. Pamoja, hatuboreshi tu miundombinu, bali pia tunaongeza uelewa wa Taifa kuhusu afya ya akili,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Delillah Kimambo amepongeza hatua ya Benki ya Exim kwa kushirikiana na kuunga mkono jitihada za kuimarisha mifumo ya afya.

“Ukarabati huu umefanyika muda muafaka, wakati changamoto za afya ya akili miongoni mwa vijana zikiongezeka nchini. Maboresho haya yatawezesha kutoa huduma bora zaidi, kwa ukarimu na heshima, kwa wagonjwa wetu,” amesema Dk Kimambo.

Jengo lililokarabatiwa lina vyumba vya wagonjwa vilivyoimarishwa, vyumba vya ushauri na tiba, maeneo ya mafunzo na ofisi za wahudumu wa afya, vyote vikiwa na vifaa vya kisasa na mpangilio mpya unaounda mazingira tulivu, salama na rafiki kwa watoto.

Mazingira haya yameundwa ili kuhamasisha uponyaji na kurejesha matumaini kwa watoto na vijana wenye changamoto za afya ya akili kipindi ambacho takwimu za idadi ya wagonjwa wa afya ya akili zikiongezeka nchini.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, idadi ya wagonjwa wa afya ya akili imeongezeka kutoka 386,000 mwaka 2012 hadi  milioni  mbili mwaka 2021, jambo linalosisitiza hitaji la haraka la kuboresha miundombinu na kampeni za uhamasishaji.

Kupitia Exim Cares, benki imekuwa ikitekeleza miradi yenye athari kubwa kitaifa, ikiwa ni pamoja na kampeni za kuchangia damu, kusaidia elimu, mafunzo ya fedha kwa wanawake na vijana kupitia Women Empowerment Programme (WEP) na kampeni za kuhifadhi mazingira.

Afya ni mojawapo ya nguzo tano za mpango huo, mingine ni elimu, mazingira, uwekezaji wa kijamii na ubunifu.