Tarime. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikihoji alipo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche, familia ya kiongozi huyo imetoa siku moja kwa Jeshi la Polisi kueleza alipo ndugu yao kabla hawajaamua kumtafuta wao wenyewe kwa kushirikiana na wananchi.
Uamuzi huo umefanywa na familia hiyo kufuatia taarifa kuwa Heche alisafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Tarime, lakini hadi sasa bado hajafikishwa na hawana taarifa rasmi kuhusu ndugu yao, huku wakidai kuwepo kwa danadana kutoka mamlaka mbalimbali.
Heche alikamatwa jana, Oktoba 22, 2025, jijini Dar es Salaam, katika viunga vya Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, alipokwenda kusikiliza kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.
Kabla ya kukamatwa, Idara ya Uhamiaji Makao Makuu ilitoa taarifa ikidai kuwa Heche alivuka mpaka kinyume cha sheria, madai ambayo Heche alikanusha akisema alikuwa nyumbani kwake Tarime, mkoani Mara.
Leo, Oktoba 23, 2025, familia ya Heche iliyopo Kijiji cha Ketagasembe, Wilaya ya Tarime, imesema imeamua kutoa muda wa siku moja ili kuonesha uvumilivu wao na kwamba hawataki kusababisha taharuki yoyote.
Mdogo wa Heche, Chacha Heche, amesema familia haiko tayari kuona ndugu yao akipoteza maisha bila sababu za msingi, kwani wanaamini hana makosa yoyote zaidi ya kuwa mstari wa mbele kudai haki na demokrasia kwa ustawi wa nchi na watu wake.
“Ndugu yetu hawezi kufa kama kuku. Ikifika kesho sisi tutaandika wosia kwa watoto wetu, tuko tayari kufa kwa ajili yake. Hawezi kufa peke yake, tunataka kujua yuko wapi hadi sasa kwani tuna wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wake na afya yake,” amesema.
Chacha amesema ndugu yao ana mfumo tofauti wa kimaisha kutokana na masuala ya usalama na afya yake, hivyo kushikiliwa kwa muda mrefu bila ndugu kujua alipo ni hatari kwa maisha yake.
“Nasema John (Heche) hawezi kufa kama kuku. Tangu jana sijala na sitakula hadi nijue ndugu yetu yuko wapi, kwani nina uhakika hata yeye huko alipo hajala chakula chochote wala kunywa maji. Hawezi kabisa kula chakula au kunywa maji atakayopewa na askari polisi,” amesema.
Amesema kwa kawaida safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Tarime huchukua saa 16 hadi 18, lakini hadi walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, zaidi ya saa 30 zilikuwa zimepita bila taarifa yoyote juu ya mahali alipo ndugu yao.
“Hatujui ndugu yetu ana hali gani yuko wapi, je, ni mzima au amekufa? Cha kushangaza, wahusika wapo kimya. Hii si sawa, waseme kama gari lao limepata changamoto njiani basi watuambie,” amesema.
Amesema ikifika kesho saa 3 asubuhi bila taarifa za alipo ndugu yao, watawashirikisha wananchi kumtafuta, na endapo hawatampata watarudi nyumbani na kutafakari hatua zaidi za kuchukua.
Chacha, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, amesema wametumia njia mbalimbali, zikiwemo rasmi za kiofisi, kiurafiki na kijamii, kujua kama ndugu yao yupo Tarime, lakini wamebaini hajaletwa.
“Bahati nzuri, kila mtu aliona Makamu Mwenyekiti akikamatwa na kupandishwa kwenye gari la polisi. Sasa tunataka kujua yuko wapi ili hatua nyingine ziendelee,” amesema Heche.
Kwa upande wake, Wakili Edward Heche, amesema baada ya kupata taarifa kuwa Heche anasafirishwa kupelekwa Tarime tangu jana, ndugu zake walijiandaa kumpokea ili wamdhamini kwa mujibu wa sheria, lakini hadi sasa haijulikani alipo.
Amefafanua kuwa, pamoja na wanafamilia wengine, wamejaribu kufuatilia alipo ndugu yao, ikiwa ni pamoja na kwenda polisi na kuonana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Mark Njera, aliyewaambia kuwa Heche hajafikishwa Tarime na hawana taarifa juu ya ujio wake.
“Nimeenda Uhamiaji, nimewasiliana na ofisa uhamiaji wa mkoa pamoja na msemaji wa uhamiaji Tanzania, wote wametoa majibu sawa kwamba hawana kesi na Heche, na wala hawamshikilii,” amesema.
Amesema awali alipowasiliana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alimuelekeza awasiliane na uhamiaji kujua alipo ndugu yao, jambo linalowafanya washindwe kuelewa nini kinaendelea kuhusu hatima yake.
Mama mdogo wa Heche, Lucia Heche, amesema ana wasiwasi na afya ya ndugu yake na kwamba kitendo cha familia kutokujua alipo kinaleta taharuki.
“Heche ana vyakula maalumu anavyotumia, sasa tangu jana hatujui yuko wapi, maana yake hajala hadi sasa. Hii ina maana hata afya yake iko mashakani, anateseka kisaikolojia na kiafya pia. Tunataka watuambie yuko wapi ili tujue tunampataje aweze hata kula,” amesema.
Amesema kitendo cha polisi kuficha alipo Heche kina madhara makubwa kwa familia, hususan mama yake mzazi ambaye ni mgonjwa, na hali hiyo inaweza kusababisha hata kifo cha mama huyo.
Chadema yahoji alipo Heche
Awali, Chadema kilihoji mahali alipo Heche, aliyekamatwa na Jeshi la Polisi katika viunga vya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, jana Oktoba 22, 2025.
Chadema kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa leo, Oktoba 23, 2025, na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, kimelitaka Jeshi la Polisi kutoa taarifa kuhusu mahali alipo kiongozi huyo.
“Leo asubuhi, timu ya mawakili pamoja na viongozi wa Chadema imefika Kituo cha Polisi Tarime kufuatilia taarifa za kukamatwa kwa Makamu Mwenyekiti Taifa. Timu yetu imeelekezwa na Polisi Tarime iende Ofisi ya Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Tarime, ambapo ilipofika ikaambiwa kuwa ofisi hiyo haijui lolote kuhusu kukamatwa au kusafirishwa kwa Heche,” imeeleza taarifa hiyo.
Kutokana na hali hiyo, timu ya Chadema ilifika Kituo cha Polisi Musoma kutafuta taarifa za Heche, lakini ikaambiwa hawana taarifa hizo.
Chama hicho kimemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillius Wambura kutoa maelezo ya haraka, ya wazi na yenye ukweli kamili juu ya mahali alipo Heche.
“Tunasisitiza, usalama wa raia hauwezi kuwa kwa maneno bali kwa vitendo. Kumficha kiongozi wa kisiasa ni uvunjaji wa haki za msingi za binadamu na ni dalili za kuendelea kuzorota kwa utawala wa sheria nchini,” kimeeleza.
Mwananchi ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pius Lutumo, kuuliza kama kiongozi huyo wa Chadema amefikishwa Mara, amesema hana taarifa hizo na kwamba Mkoa wa Mara una mikoa miwili.