Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imeipokea nakala ya maelezo ya maandishi ya shahidi wa tatu wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kuwa kielelezo cha upande wake.
Mahakama hiyo imepokea na kusajili maelezo hayo ya shahidi huyo wa tatu wa Jamhuri kuwa kielelezo cha upande wa utetezi katika kesi hiyo, leo Alhamisi, Oktoba 23, 2025, kufuatia maombi ya Lissu kwa shahidi huyo, naye akakubali kuyatoa.
Lissu ameiomba mahakama iyapokee maelezo hayo kuwa kielelezo cha upande wake ili ayatumie kujitetea, kwa kumuhoji maswali ya dodoso kwa lengo la kuonesha kukinzana kwa ushahidi wake huo wa maandishi na ule wa mdomo alioutoa kizimbani chini ya kiapo.
Katika kesi hiyo namba 19605 ya mwaka 2025, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha maneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”.
Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde ipo katika hatua ya ushahidi wa Jamhuri, ikiwa ni shahidi wa tatu.
Shahidi huyo wa tatu ni Mkaguzi wa Jeshi Polisi, Samweli Kaaya (39), Mtaalamu wa picha, kutoka Kitengo cha Picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai. Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake wa msingi alieleza kuwa Aprili 8, 2025 alipokea ‘flash disk na memory card’ zenye video ya Lissu yenye maudhui yanayodaiwa kuwa ya uhaini, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Dar es Salaam kuchunguza uhalisia wake.
Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa katika uchunguzi wake alibaini kuwa video hiyo ni halisi na haina pandikizi, kisha akaandaa ripoti ya uchunguzi huo.
Jana Oktoba 17, 2025 aliiomba mahakama hiyo ivipokee vihifadhi data hivyo (flash disk na memory card) zenye video ya Lissu, lakini Lissu aliiwekea pingamizi na Mahakama katika uamuzi wake jana Jumatano ilikubaliana na pingamizi hilo ikavikataa vihifadhi data hivyo.
Baada ya uamuzi huo Jamhuri iliomba ripoti ya uchunguzi wa uhalisia wa video hiyo alioufanya shahidi huyo ipokelewe kuwa kielelezo cha ushahidi wa Jamhuri, pia Lissu akaipinga na Mahakama katika uamuzi wake leo, imekubaliana na pingamizi la Lissu na kuikataa ripoti hiyo.
Kama mahakama ingekubali kuipokea ripoti hiyo, shahidi huyo angeendelea na ushahidi wake wa msingi, kwa kusoma ripoti hiyo kwa sauti na kisha kuzitolea ufafanuzi wa matokeo ya uchunguzi huo, lakini uamuzi huo wa kuikataa ndio umehitimisha ushahidi wake wa msingi.
Baada ya uamuzi huo mwendesha mashtaka aliyekuwa akimuongoza shahidi huyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawab Issa ameieleza mahakama kuwa huo ndio mwisho wa ushahidi wake kwa upande wao na sasa yuko huru kwa ajili ya maswali ya dodoso.
Hivyo Lissu ameanza kumuhoji kama aliandika maelezo yake kuhusiana na jukumu alilolifanya katika kesi hiyo na shahidi huyo akakubali kuwa aliandika.
Lissu : Shahidi, uliandika maelezo polisi?
Lissu: Ni kweli uliandika maelezo hayo Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi, Makao Makuu Dar es salaam Aprili 8, 2025?
Lissu: Na maelezo yako iliyaona utayatambua?
Baada ya maswali hayo, Lissu ameiomba mahakama, Jamhuri impatie maelezo hayo ili amuoneshe shahidi ayatambue.
Amedai kuwa kuna maeneo ambayo anataka kumuuliza maswali ya dodoso kuhoji kuaminika kwake kwa kuonesha maeneo yanayokinzana na ushahidi wake wa mdomo, na shahidi huyo alipopewa ameyatambua kuwa ndiyo maelezo yake aliyoyaandika.
Kisha Lissu ameyasoma yote kwa sauti kisha akaanza kubainisha maeneo ambayo aliyodai kuwa yanakinzana na ushahidi wa mdomo wa shahidi ambapo ameainisha maeneo 75.
Baada ya kuainisha maeneo hayo amemuuliza shahidi kama angependa kuyawasilisha mahakamani yapokewe kuwa kielelezo naye shahidi akakubali.
Upande wa mashtaka ulipoulizwa na Mahakama kama wana jambo lolote kuhusiana na kupokewa kwa maelezo ya shahidi wake huyo kuwa kielelezo cha upande wa utetezi.
Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Lenatus Mkude amesema kuwa hawana pingamizi na maelezo hayo kupokewa kuwa kielelezo cha upande wa utetezi.
Kutokana na maelezo hayo ya upande wa mashtaka, Jaji Ndunguru amesema kuwa maelezo hayo ya shahidi namba tatu wa upande wa Jamhuri yamepokelewa na kuwa kielelezo cha pili cha upande wa utetezi.
Bada ya maelezo hayo kupokewa mahakamani na kuwa kielelezo cha upande wa utetezi, Lissu akaanza kumuhoji maswali kuhusiana na maelezo hayo aliyoyaandika dhidi ya ushahidi wake wa mdomo.
Katika maswali hayo Lissu amejikita katika maelezo aliyoyatoa shahidi katika ushahidi wake wa mdomo kizimbani kuhusiana na elimu yake, taaluma na ujuzi wake pamoja na taratibu za utekelezaji wa majukumu yake kama yapo kwenye maelezo ya maandishi.
Hata hivyo, katika maswali mengi shahidi huyo amejibu kwenye maelezo yake ya maandishi hayapo, huku katika maswali machache akijibu kuwa hajui na mengine machache hasa uliyohusu ujuzi wake akiyatolea ufafanuzi.
Pia Lissu amemuuliza maswali kadhaa yasiyohusiana na maelezo ambayo hayako kwenye maandishi.
Hata hivyo, upande wa mashtaka katika maswali ya kusawazisha majibu ya shahidi kwa maswali ya Lissu, umemuuliza swali moja tu ambalo jibu lake ametoa ufafanuzi uliojibu maswali yote yaliyohusu maelezo yake ya ushahidi wa mdomo ambayo hayako kwenye maelezo ya maandishi.
Katika ufafanuzi wake amesema kuwa maelezo ya maandishi ni muhtasari tu wa kile alichokifanya na asingeweza kuandika kila jambo, kwani hayo yasingekuwa maelezo ya ushahidi bali ingekuwa ripoti ya utafiti au kitabu.
Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho kwa ajili ya kuendelea na shahidi mwingine wa Jamhuri atakayekuwa ameandaliwa.