Jinsi wateja wanavyoomba keki, vinywaji vyenye dawa za kulevya

Dar es Salaam. Wakati vijana wa vyuo vikuu wakituhumiwa kutengeneza biskuti za bangi, wapishi na watengeneza vinywaji jijini Dar es Salaam wamesema wamekuwa wakiombwa na waandaji wa sherehe kuweka dawa za kulevya kwenye keki na vinywaji ili wageni wajisikie vizuri.

Wapishi hao wamesema vitendo hivyo vinaashiria kuwa, kila siku watumiaji wanatafuta njia mbadala za kutumia dawa za kulevya kupitia sherehe, jambo linalohatarisha afya na maadili ya jamii.

Wakati hayo yakiendelea, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeanzisha mpango maalumu wa kufanya ukaguzi wa vinywaji na vyakula vinavyotumika katika sherehe mbalimbali zikiwamo za nyumbani na ukumbini.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Oktoba 22, 2025 mpishi wa vyakula ambaye ameomba hifadhi ya jina lake, amesema amewahi kukosa kazi baada ya kukataa ombi la kutengeneza keki yenye bangi.

“Kuna mteja alinipigia simu akaniambia anataka ‘spice cake’. Nilipomuuliza maana yake, akasema ni keki yenye bangi kidogo ili wageni wake wajisikie vizuri. Nilimwambia siwezi kufanya hivyo alinijibu, basi tutatafuta mwingine,” amesema mpishi huyo.

Amesema ombi kama hilo linaonesha jinsi baadhi ya vijana wanavyokosa uelewa wa madhara ya dawa za kulevya, na kwamba wapishi wanapaswa kuwa walinzi wa maadili ya jamii.

Mpishi huyo amesema maelezo aliyopewa ni kuwa, baadhi ya vijana waliozoea kutumia dawa za kulevya, hujihisi hawapo huru na kuzubaa katika sherehe, hivyo wanahitaji kichangamsha mwili na akili.

“Wengine hushindwa kuvuta bangi hadharani, hivyo hutumia mbinu kama hizi. Wanaomba wapishi tuwasaidie kutengeneza keki au vinywaji vyenye kilevi. Lakini  binafsi siwezi kufanya hivyo, maana najijengea jina la kazi, sifanyi vitu vya kuhatarisha heshima ya kampuni yangu,” amesema.

Neema Shaweji, mpishi wa vitafunwa anayehudumia hafla mbalimbali, amesema baadhi ya wateja wanatoa maelekezo ya wazi ya kutaka keki au kashata zenye bangi, wakidai zinasaidia kuondoa msongo wa mawazo.

“Wengine wanakuambia tuna marafiki zetu wanatumia, wacha ‘wa-enjoy’ na wanakutaka usiweke nyingi huku wengine wakihitaji usiri bila wageni kufahamu chochote, jambo ambalo ni la hatari zaidi,”amesema Neema.

Mtengeneza vinywaji (mixologist), Bahati Mrope amesema changamoto kama hiyo ipo pia kwa upande wa vinywaji, wateja huomba dawa za kulevya zichanganywe kwenye pombe au ‘Cocktails.’

“Wapo wanaoniambia niweke kitu kidogo kwenye Cocktail zao ili wageni wafurahi. Wakati mwingine nakataa, lakini kutokana na ofa ninayopewa siwezi kuacha pesa japokuwa ni kinyume cha maadili na sheria,”amesema Bahati.

Amesema kuna makosa mengi wanayafanya bila wao kujua kuwa wanahatarisha maisha ya watu, kwa sababu wapo wengine ni wagonjwa wanaposhiriki kwenye sherehe na kunywa vinywaji vyenye dawa za kulevya ni kuwaongezea ugonjwa zaidi.

Neema ametoa wito wa kutotumia vinywaji ambavyo mtu hajawahi kutumia kwa kuwa, inaathari kubwa, hivyo wanatakiwa kuendeleza utamaduni wa vinywaji vyao.

“Niwaombe watu wanaokwenda kwenye sherehe za ndani kuacha kutumia vinywaji wanavyoviona mara ya kwanza, kwa madai wanafanya majaribio kufahamu ladha yake hususani hivi visivyotoka viwandani kwa kuwa vina vitu vingi,”amesema Neema.

Hata hivyo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo  ameeleza mpango maalumu wa kufanya ukaguzi wa vinywaji na vyakula vinavyotumika katika sherehe mbalimbali, kufuatia ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya katika vyakula na vinywaji hivyo, bila uelewa wa watumiaji.

Amesema mpango huo utahusisha uchunguzi wa vinywaji vyote vinavyotengenezwa kienyeji  katika shughuli za kijamii ili kubaini kama vina viambata vinavyohusiana na dawa za kulevya.

“Kuanzia sasa, tutakapokwenda kwenye sherehe yoyote na kukuta kinywaji cha kutengenezwa, tutakipima. Tukibaini kina viambata vya dawa za kulevya, huyo mtengenezaji atashitakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi,” amesema Lyimo.

Ameeleza kuwa, baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vyakula kama keki na vinywaji vilivyowekwa bangi, mirungi au kemikali za kulevya kama sehemu ya starehe, hali ambayo imekuwa na madhara makubwa kiafya, hasa kwa watu wenye shinikizo la damu, kisukari au magonjwa ya moyo.

“Matumizi ya dawa za kulevya huathiri ubongo na kuongeza mapigo ya moyo. Wenye maradhi wanapokula au kunywa chakula chenye dawa hizo hupata mshituko wa moyo au kifo cha ghafla,” amesema Lyimo.

Mbali na hilo, amesema kumekuwa na matumizi ya mafuta ya kupaka ambayo yanatengenezwa kienyeji kwa kuchanganya na bangi kwa kuaminishana kuwa, hayana madhara, akisema si salama na watawachukulia hatua.

Kamishna Lyimo ameonya watengenezaji wa vinywaji na vyakula vya sherehe vinavyochanganywa na dawa kuacha utengenezaji wa bidhaa zenye viambata hatarishi, akisema mbali na adhabu ya kifungo kirefu, bidhaa hizo zitataifishwa na biashara kufungwa.