Kampeni za udiwani Kirua Vunjo Magharibi zatishiwa kufuatia kifo cha mgombea

Moshi. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesitisha shughuli zote za kampeni za uchaguzi wa udiwani katika Kata ya Kirua Vunjo Magharibi, Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, kufuatia kifo cha mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), John Kessy.

Kessy alifariki dunia Oktoba 21, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi iliyopo Manispaa ya Moshi.

Akizungumza leo Oktoba 23, 2025 kuhusu kusitishwa kwa uchaguzi huo, Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Vunjo na Moshi Vijijini, Lucas Msele amesema kifo cha mgombea kinapotokea, shughuli zote za uchaguzi husitishwa hadi utakapopangwa utaratibu mwingine na INEC.

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Vunjo na Moshi vijijini, Lucas Msele akizungumzia kuhusiana na kusitishwa uchaguzi katika kata ya Kirua Vunjo Magharibi.

“Nimepokea barua kutoka kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi ikitujulisha kuhusu kifo cha mgombea udiwani wa Kata ya Kirua Vunjo Magharibi kilichotokea Oktoba 21, 2025 katika Hospitali ya Mawenzi,” amesema Msele.

Amesema baada ya kupokea taarifa hizo, ofisi yake ilitoa taarifa kwa umma kuhusu kusitishwa kwa shughuli zote za uchaguzi katika kata hiyo.

“Kwa sasa, tunasubiri maelekezo kutoka INEC kuhusu utaratibu wa uteuzi wa mgombea mwingine na lini kampeni pamoja na shughuli za uchaguzi zitarejelewa,” ameeleza msimamizi huyo wa uchaguzi.

Aidha, Msele amesema taarifa rasmi kuhusu tarehe mpya za uteuzi, kampeni na uchaguzi zitatolewa kupitia Gazeti la Serikali baada ya INEC kukamilisha taratibu husika.

Kwa mara ya kwanza mgombea huyo alichaguliwa kuwa diwani mwaka 2020 na 2025 alikuwa akigombea kipindi chake cha pili.