Khambay anatosha Babati mjini – Sumaye

Babati. Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amewasihi wakazi wa mjini Babati mkoani Manyara, kumpa kura za ndiyo mgombea ubunge kupitia CCM, Emmanuel Khambay kwani atayafikia makundi yote.

Sumaye ameyasema hayo kwenye kata ya Bonga mjini Babati wakati akiwanadi wagombea wa CCM akiwamo mgombea urais, Samia Suluhu Hassan, ubunge na udiwani.

Amesema mgombea ubunge kupitia CCM Khambay anatosha kuwatumikia wana Babati mjini kwani ameonyesha mfano kwa kuwafikia makundi yote, hivyo hana ubaguzi.

“Mmeona kwenye kampeni za CCM, Khambay ametembelea makundi yote ya bodaboda, sokoni, mama na baba lishe, wavivu, wakulima, wafugaji, vijana, wazee na watu wenye ulemavu,” amesema.

Pia, Sumaye amewaombea kura mgombea urais wa CCM Samia pamoja na mgombea udiwani wa kata ya Bonga Hiiti.

“Msisahau kumpa kura mgombea urais wa CCM mama yetu Samia Suluhu Hassan kwani ni kipenzi cha Watanzania aliyefanya mambo mengi na makubwa,” amesema Sumaye.

Kwa upande wake, Khambay amewaomba wakazi wa kata ya Bonga kumpa kura zote za ndiyo ili aweze kuwatumikia wananchi wa Babati mjini.

Amesema ana historia nzuri ya uongozi tangu akiwa mdau wa maendeleo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM mjini Babati, hivyo uongozi anaufahamu haendi kujifunza.

“Mafiga ni matatu kama kawaida tunaomba kura za mgombea urais, Samia Suluhu Hassan, mimi mbunge wenu Khambay na mgombea udiwani hapa Bonga Hiiti, siku ya Jumatano ijayo Oktoba 29 mwaka 2025 tujitokeze kwa wingi tukapige kura,” amesema Khambay.

Katibu mwenezi wa CCM Mkoa wa Manyara, John Nzwalile amesema Khambay ni kiongozi ambaye hana ubaguzi katika kuwatumikia wananchi.

Nzwalile amempongeza Khambay kwa kufanya kampeni nzuri na kujitahidi kuyafikia makundi mengi mjini Babati hivyo ni mtu sahihi.

Mgombea udiwani wa Kata ya Bonga, Hiiti amewaomba wakazi wa eneo hilo kumpa kura nyingi za ndiyo ili aweze kuongoza kwa kipindi kingine cha tatu.

Amesema wana Bonga wameanza kumpa heshima yake kuanzia mwaka 2015/2020 kisha 2020/2025 na sasa 2025/2030 anatarajia watampa heshima hiyo tena.