Madereva bodaboda, bajaji wafundwa kupambana na rushwa

Mwanza. Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, Crispin Francis amewataka wasafirishaji abiria wakiwemo madereva pikipiki (bodaboda) na bajaji kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.

Crispin ametoa wito huo leo Oktoba 23, 2025 jijini Mwanza wakati akizindua machapisho ya sera ya taasisi hiyo kupitia kampeni ya ‘Takukuru tupo site’ yenye lengo la kuendelea kuongeza jitihada na nguvu katika kupambana na kuzuia vitendo vya rushwa mkoani Mwanza.

Amesema elimu hiyo inayotarajiwa kuzinduliwa nchi nzima inalenga kutoa elimu na kufikisha ujumbe kwa jamii kupambana na rushwa kupitia wadau wakiwemo madereva bodaboda na bajaji, ili kuhakikisha kila mtu anakuwa na utambuzi kuhusiana na vitendo vya rushwa na madhara yake.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, Crispin Francis akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya sera ya Takukuru tupo site, leo katika ofisi za taasisi hiyo jijini Mwanza. Picha na Eliezel Mgeta

Mkurugenzi huyo amesema wameamua kutoa elimu hiyo kwa maofisa hao ili kuwaeleza madhara yanayoweza kutokana na vitendo vya rushwa na mbinu za kukabiliana nayo.

“Tumeamua kushirikiana na madereva wa vyombo vya usafirishaji bodaboda na bajaji kwani wanatumika katika kusafirisha watu mbalimbali hivyo kupitia wao tunaweza kufikisha ujumbe wa kuzuia na kupambana na rushwa kwa urahisi na haraka zaidi katika jamii,” amesema Crispin.

Crispin amewaomba madereva hao kuhakikisha wanashirikiana na taasisi hiyo ili kuisaidia jamii kuepukana na vitendo vya rushwa hususan wakati huu wa kampeni za uchaguzi mkuu kwa kutoa elimu ambayo wao wameipata.

Ofisa Tawala Wilaya ya Nyamagana, Tausi Mvango, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Amina Makilagi, amesema Serikali itaendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya rushwa,  kwani ni chanzo cha uvunjifu wa amani katika jamii.

“Sisi kama sehemu ya jamii ya Mkoa wa Mwanza tutaendelea kuihamasisha jamii kuhakikisha inapinga na kuzuia rushwa, pia nipongeze juhudi na jitihada zinazoendelea kufanyika ili kuzuia vitendo vya rushwa kwani rushwa ni chanzo kikubwa cha uvunjifu wa amani na umoja katika jamii,” amesema Mvango.

Mwenyekiti wa Waendesha Pikipiki (Bodaboda) Mkoa wa Mwanza, Mohammed Iddi amesema kuwa kupitia fursa kubwa waliyonayo ya kufikia idadi kubwa ya watu watahakikisha wanaunga jitihada zinazoendelea kufanywa na Takukuru ili kuzuia rushwa, kwa kutoa elimu kwa kila abiria watakayembeba kuhusu madhara yatokanayo na rushwa.

Mwenyekiti wa waendesha bajaji Mkoa Mwanza, Mansour Ahmada amesema kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anapinga na kuzuia vitendo vya rushwa ili kujenga jamii imara yenye upendo na umoja, hivyo, waendesha bajaji wapo tayari kusambaza elimu hiyo kwa jamii nzima, ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.