MGOMBEA UBUNGE CCM KUJENGA GHOROFA SHULE ALIYOSOMA

Wa pili Kushoto ni Mgombea Udiwani wa kata ya Bwera,Josephat Manyenye akiwa na Mgombea Ubunge Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula (wa tatu kutoka Kushoto)
 :::::::::::

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula, ameahidi kujenga madarasa na Ofisi ya walimu kwenye shule ya msingi aliyosomea.

Amesema shule ya msingi Igando ndiyo iliyomsaidia kupata maarifa na kwamba kamwe hawezi kushindwa kurudisha fadhira iwapo wananchi wa Jimbo hilo watamchagua kuwa Mbunge wao.

“Ninakusudia kujenga madarasa na Ofisi ya walimu kwenye shule niliyosomea, natambua shule ya msingi Igando jinsi ilivyonifanya kuwa hivi nilivyo sasa, lakini ili hilo lifanikiwe nimuhimu sana mumpigie kura nyingi Dkt. Samia ili awe Rais, na mimi niwe Mbunge na Manyenye kuwa diwani wenu” amesema Lutandula.

Alikuwa kwenye mkutano wa kampeni kwenye Kijiji cha Igando kata ya Bwera Jimbo la Chato kusini, huku akiwahimiza Oktoba 29 mwaka huu kuamka asubuhi na mapema ili kwenda kutimiza haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Mbali na hilo, pia amewasihi kuacha kuuza ovyo ardhi zao kwa bei ya hasara badala yake wasubiri akiapishwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo ili maeneo hayo yapimwe kitaalamu na kuyaongezea thamani kwa madai yajayo yanafurahisha.

Amesema ardhi ambayo haijapimwa haiwezi kuwa na thamani kubwa ukilinganisha na iliyopimwa na kwamba ili waweze kupata tija ni muhimu sana ardhi hiyo kuongezewa thamani.

Kadhalika ameahidi kufungua barabara za mitaa kwa kiwango cha changarawe ili kurahisisha mawasiliano pamoja na kusafirisha mazao ya wakulima kutoka mashambani.

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Bwera, Josephat Manyenye, amewakumbusha wananchi baadhi ya miradi ya maendeleo aliyoitekeleza kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita huku akiwaomba kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu aweze kuendeleza alipokomea.

Amesema hana shaka na mahitaji ya wananchi hao kwa madai anazitambua shida zao kwa madai ni mtoto wao na mwenye kuyajua matatizo ya jamii hiyo.

Diwani huyo anayekumbukwa na Baraza lililopita la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita kutokana na kuibua mjadala wa kutaka kugawanywa kwa Jimbo la Chato ili yapatikane mawili, amesema anatambua namna ya kujenga hoja zenye maslahi mapana kwa jamii ili kuwaletea maendeleo wananchi hao.




                        Mwisho